Bahati mbaya sana kwa wakazi wa dunia kila mpango wa uliofanywa na maadui zetu unakwenda kama wanavyo taka wao, New World Order iko wazi, lakini ni kwa wale walio huru kiakili ndiyo wanayo weza kuiyona, wengine tunasubiri itangazwe rasmi. Lakini nikipi hicho kilichoko kwenye New World Order?

Mpango mchafu, mweusi mbaya na hata usiofikirika kwa mtu wa kawaida ni KUPUNGUZA idadi ya watu duniani kwa asilimi 90! Iliasilimia 10 itakayo baki iwiane vizuri na mazingira yake. Kwa kutumia njia mbaya na kushinda mnyama. Hapo utakutana na Nyota ya Kijani, Mpango wa uzazi salama, elimu ya ngono mashuleni, vyakula na madawa yanayotiwa dawa na visababishi vya ugumba kwa siri, virusi na maradhi ya kutengeneza maabara kama ebola, ukimwi, chanjo za aina kwa aina, vita kila kona ya dunia na mapango wa WWIII, ukame na majanga mengine ya kutengeneza tunayo dhani ni ya asili.

Kisha idadi ya watu inayotakiwa ikisha fikiwa ajenda itawekwa hadharani ikiwa na Serikali Moja ya Dunia (Serikali ya Kishetani), Dini moja kwa watu wote (Dini ya Kumuabudu Shetani) Jeshi Moja la Dunia (Kwa ajili ya kupambana na wale watakao taka kuipindua serikali hiyo) Sarafu moja kwa dunia nzima, na wananchi wote wakuwa na Microchip kwa ajili ya kufuatilia nyendo za kila raia masaa 24/7.

Kifupi ni kuuwa asilimia 90 ya binadamu wote, na kutawala nyanja zote za maisha, na kumtawala kila mtu na kila kitu kutoka siku unazaliwa mpaka unaingia kaburini!

Wakati unafikiri hilo haliwezekani mpango huu umeshakamilika kwa zaidi ya asilimia 90%

NAIKUBALI HII

NJIA YA MATUMAINI KWA TEJA WA PORNOGRAPH

Hichi ndicho anachokisema Mwanasaikriatiki wetu Norman Doldge, “Ukurasa wa nyuma kwenye jarida la wanaume liitwalo Risque na kuras...

Tuesday, April 19, 2016

NAMTAFUTA MUNGU Ep: 5


Hıvyo Uislamu maana yake ni salama, amani, kujisalimisha. Unapokuwa Mwislamu inaamanisha kuwa wewe umechagua kujisalimisha kwenye sheria za MUNGU MMOJA.



Kwenye mafundisho yake yote ambayo aliyaleta kupitia mitume mbalimbali, na Quran yenyewe imetaja habari za mitume 25, na mafunzo ya mtume Muhammad Rehmana Amani iwe juu yake yanatufundisha kuwa walipatikana mitume wafikao laki moja na ishirini na nne elfu. Kwa zama mbalimbali sehemu mbalimbali duniani walipatikana mitume wa MUNGU MMOJA. 

Hıvyo kama tunaweza kuipata historia ya kweli ya jamii mbalimbali duniani tutakuta kuwa, Wapare, Wachaga, Wamasai, Wakikuyu Wachina, Wazulu, wasandawe na wengine na wengine kihistoria katika nukta fulani ya historia yao, walipata kuwa na mitume wa kweli kutoka kwa MUNGU MMOJA ambao waliwafundisha maneno yaleyale, yanayo patikana kwenye Zaburi, ya Mtume Daud (David), Torati ya mtume Musa (Moses), Injili ya Mtume Isa (Yesu) na Quran ya mtume Muhammad wote Rehma na Amani ziwe juu yao, nayo si mengine ila Mungu, Bwana wetu ni MUNGU MMOJA.

Hıvyo Uislamu siyo dini mpya, siyo dini iliyo anzishwa na Muhammad takribani miaka 1400 iliyo pita. Hapana, Uislamu ulikuwepo tangu binadamu wa kwanza, Adam, Rehma na Amani ziwe juu yake, alipo kanyaga dunia, naye ndiye binadamu wa kwanza Mwislamu, dai hili linathibitishwa na vitabu mbalimbali, ikiwemo vitabu halisi vya MUNGU MMOJA ambavyo walipewa mitume mbalimbali, kwa uchache hapo juu tumeona matendo yaliyo kuwa yanafanywa na Musa (Moses), Isa (Yesu), Amani ya Mungu iwe juu yao, ndiyo matendo yaleyale aliyo yafanya Muhammad na ndiyo yanayo fanywa na wafuasi wa Muhammad kote duniani. Utaona Uislamu ndiyo dini ya paekee ambayo inawakubali mitume wengine walio tangulia, akiwemo Issa/Yesu mwenyewe na mafundisho yake sahihi.

Katika dunia ya leo, ambayo mwelekeo wake na muongozo wake umeegemea kwenye kile kinacho itwa ‘sayansi,’ na ambapo jambo lolote ambalo litaletwa katika jamii ya leo bila kukidhi vigezo na kanuni za kisayansi, halitakuwa na mvuto na litaonekana kama ni upuuzi mtupu. Katika hili vitabu vya MUNGU MMOJA navyo havikuwa nyuma, vimethibitisha kile ambacho hata sayansi bado iko mbali sana kuvijibu au kuvigundua. Kwenye hili ningependa kutumia kitabu kimoja tu, cha MUNGU MMOJA, ambacho hakijatiwa mikono ya mtaalam binadamu tangu kilipo teremshwa kwa mtume wake Muhammad Rehma na Amani ziwe juu yake.



Kitabu cha dini ya MUNGU MMOJA, hakiwezi kupingana na sheria za kimaumbile za ulimwengu, zilizo wekwa na MUNGU huyohuyo. Lakini kuzaliwa kwa ‘wale’ ambao wanajitangaza kama wanasiasa kali, na kujipachika cheo cha; ‘wasemaji wa Mungu,’ na wanasayansi ambao wanafanya kila wawezalo kutafuta mgongano baina ya vitabu vya MUNGU MMOJA na kanuni za maumbile, kuna waacha njia panda wale ambao bado wanautafuta ukweli, na ambo kwa bahati mbaya nyenzo za kutekeleza jukumu hilo ni duni kwa kila hali.

Tunapo kitazama kitabu cha Quran, hakina mfano, namna vile ambavyo chenyewe kinavyo simama dhidi ya ‘wasemaji wa Mungu’ na wanasayansi wa kimaterialisim, na binadamu wote kwa ujumla, kiasi kwamba udhati wake unawafanya wote, waumini na wasio waumini, waone juu ya yote kitabu hichi ni tofauti sana dhidi ya vitabu vingine.

“Au wanasema: Ameghushi? Sema: Basi leteni Sura kumi zilizo ghushiwa mfano wa hii, na waiteni mwawezao badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli. Na wasipo kuitikieni, basi jueni ya kwamba (hii Qur’an) imeteremshwa kwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu, na kwamba hapana mungu ila Yeye. Basi je! Mutakuwa Waislamu?” (Quran 11: 13-14)

Quran inatoa changamoto kwa wale ambao wanao sema kuwa kitabu hichi amekiandika Muhammad mwenyewe, wanao dai kuwa Muhammad ameghushi hichi kitabu. Basi walete japo sura kumi tu mfano wa Quran ikiwa madai yao ni ya kweli. 

Ikiwa Muhammad, binadamu kama binadamu wengine ameweza kughushi hichi kitabu, basi uwezekano wa binadamu wengine kufanya hivyo upo, ndipo Quran inapoweka wazi hiyo changamoto yake kwa hao wenye dai hilo, kwamba na nyinyi andikeni basi japo sura kumi tu mfano wake. Lakini Quran haijaishia hapo tu, inawataka hao wenye dai hilo wawaite wowote wale wawatakao ambao wanadhani wanaweza kuwasaidia kufanyiza Sura kumi tu, mfano wa Quran. Kitabu cha Quran kina jumla ya sura mia moja na kumi na nne, lakini changamoto imetolewa japo kwa sura kumi. 

Tangu changamoto hiyo itolewe, leo ni zaidi ya miaka 1400, na hakuna yeyote, si katika majini wala binadamu au wote kwa pamoja walio jitokeza na kuweza kufanyiza sura kumi tu mfano wa hizo kwenye Quran. Unadhani wangeweza kufanyiza ni makelele kiasi gani wangepaza kupitia mitandao ya vyombo vya mawasiliano wanavyo vimiliki? Lakini ni zaidi ya miaka 1400 na wote wapo kimya! Kina nini kitabu hichi hata washindwe?

“'Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyo mteremshia mja wetu basi leteni sura moja ya mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli.”
“Na ikiwa hamtofanya - na wala hamtofanya kamwe - basi uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe na walio andaliwa (moto) huo ni wanao kanusha.” (Quran 2: 23-24)

Changamoto imetajwa tena hapa, lakini hapa, wanaambiwa wakanushaji, walau walete sura moja, siyo kumi tena, basi leteni hata moja ya kughushi, ikiwa hayo mnayo sema ni ya ukweli kwamba Muhammad kaghushi, basi na nyinyi ghushini japo sura moja tu. Lakini Quran inawaonya kwa kiburi chao hicho na inawathibitishia kuwa hawato weza kughushi hata hiyo sura moja! Hichi ni kitu cha ajabu mno, ni vipi Muhammad alijua karne zitakazo fuata baada ya kuondoka kwake hakuna atakaye weza kuandika japo sura moja mfano wa hii Quran? Na kama wataendelea na kiburi chao, cha kufungia jicho huu ukweli ulio wazi kama jua la saa sita lisilo na wingu, basi adhabu yao ni moto ambao kuni zake moto huo ni watu wenyewe pamoja na mawe. (Mungu tuhifadhi na adhabu ya Moto, kwa hakika adhabu yako ni kali mno na umewaandalia wakanushaji)

Historia mpaka leo, ni shahidi kuwa hakuna yeyote aliyeweza kughushi japo sura moja, achilia mbali kumi. Hapana shaka makafiri wanao mkaanusha MUNGU MMOJA, ikiwa katika lolote ambalo wangeweza kulifanya, kuligharamikia kwa kila senti waliyo nayo, kwa kila uhai walio nao, kwa kila maarifa waliyo nayo na kwa kila rasilimali waliyo nayo, basi ilikuwa ni kughushi japo hiyo sura moja, ili waseme maneno ya Muhammad yameanguka patupu. Lakini imebaki ni nia na hamu tu yakutaka kufanya hivyo, na leo ni zaidi ya miaka 1400 na bado hawajaweza. Na MUNGU MMOJA kesha sema hawato weza, basi na waogope adhabu zake.

“Sema: Wangelikusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii Qur’an basi hawaleti mfano wake, hata wakisaidiana wao kwa wao.”(Quran 17: 88)

Hapa tena Mola Mtukufu anarudia kuwaambia wale waliokufuru, wale wanaoipinga haki, wale wanao sema kuwa Muhammadi ameghushi kitabu hicho, kwamba hata ikibidi wakusanyike binadamu na majini, ili waweze kutengeneza mfano wa hii Quran, bado hawato weza. Majini ambao ni washirika wakubwa wa binadamu katika mambo, mbalimbali, ukizingatia na wao ni viumbe huru kama wanadamu, na zaidi ya hapo majini walikuwepo kwenye mgongo huu wa aridhi kwa kipindi kirefu kabla ya kuja mwanadamu, na ushahidi wa kazi zao upo tukipata wasaaa tutazirusha hapa pia, na hivyo kama ni msaada kutokana na uzoefu wa wao kuwepo hapa kwa muda mrefu, basi wanao wa kutosha, basi na washirikiane na binadamu katika kutengeneza mfano wa kitabu hichi, tangu na tangu mpaka leo hakuna walio jitokeza kufanya hivyo.

Ikiwa Muhammad ndiyo mwandishi wa kazi ni wapi alipata ujasiri wa kutamka maneno hayo, na vipi maneno hayo yaweze kusimama dhidi ya changamoto za zama hadi zama. Lakini Muhammad mwenyewe hajasema kuwa hiyo ni kazi yake, mara zote alisema kuwa yeye ni mjumbe tu, na hasemi ila lile ambalo MOLA wake amemuamrisha kusema. Wamepita wanafalsafa, wanasayansi, wanajimu, wanafizikia na wanataaluma mbalimbali ambao kazi zao zimeweza kutambulika na kutunukiwa nishani mbalimbali, lakini hakuna kati yao aliyesema kazi hiyo ni ya fulani, kila mmoja alikiri ni ya kwake na akatambulika kwayo. Ila Muhammad yeye amesema kazi hiyo si yake, yeye ni mjumbe tu.

Lakini juu ya yote Muhammad mwenyewe hakuwa akijua kusoma wala kuandika. Ni vipi mtu kutoka katika jangwa la Arabia karibu milenia moja na nusu iliyo pita, asiye weza kusoma wala kuandika, aje na kazi ambayo hata leo kwenye zama za sayansi na teknolojia, zama zilizo shuhudia ufanisi wa hali ya juu na tafiti zilizo kidhi haja na viwango, zama zilizo na wanasayansi na watafiti wa aina kwa aina zishindwe kuyaangusha maneno aliyo yasema? 

Zishindwe kuja na walau sura moja mfano wa hiyo Quran? Inayo kitu gani hii Quran iliyo andikwa kupitia kinywa cha Muhammad kiasi kwamba hata wakikusanyika watu na majini, wote kwa pamoja hawawezi kuleta mfano wake, mfano wa kitabu kilicho kuja kupitia mtu asiye fahamu kusoma wala kuandika?
Ningeomba kuchukua nafasi hii adhimu mno, tupitie baadhi ya nukta chache ndani ya kitabu hicho kitakatifu, chache tu.[1]

“Na mbingu tumezifanya kwa nguvu na uwezo na hakika Sisi bila ya shaka ndio wenye kuzitanua.” (Quran 51: 47)

Ulimwengu ukoje? Ni swali ambalo tangu historia ya awali ya binadamu inarekodiwa, swali hili, liliweza na bado linaendelea kuzigusa akili za wanafalsafa, wanafizikia na wanajimu kutaja kwa uchache. Liligusa bongo kubwa za wanafalsafa kabla halijapata njia kwenye sayansi ya fizikia. Wako waliyo ona kuwa ulimwengu hapo ulipo ndivyo ulivyo, na wapo waliofikiri zaidi ya hivyo. Quran ina utaja ulimwengu kwamba unapanuka.

Upande mmoja tunaye Muhammad jangwani, siyo mwanafizikia wala mwanafalsafa, hajui kusoma wala kuandika na kwa upande mwingine, tunayo maono na mitazamo ya bongo nzito nzito kama vile Aristotle, Ptolemy, Giordano Bruno, Galileo Galilei na Isaac Newton kutaja lakini kwa uchache. Bongo hizo dai lao limeegemea kwenye tafiti, uchunguzi, kanuni za kimahesabu, ukusanyaji wa taarifa na takwimu za muda mrefu, zingine hata kabla wao hawajazaliwa, wakidai kuwa eidha ulimwengu upo kama ulivyo umetulia au ulimwengu ni tufe lenye nafasi isiyo na mipaka, lakini haikupita kwenye akili ya mmoja wao, kufikiri kuwa ulimwengu upo kwenye hali ya kuendelea kutanuka. Mpaka kwenye karne ya 20, pale Edwin Hubble, kwa msaada wa kifaa kinacho fahamika kama teleskop, alipo weza kubainisha kuwa ulimwengu unatanuka daima. 


Nadharia hii ya kuwa ulimwengu upo kwenye hali ya kutanuka ilianza kushika kasi kwenye miaka ya 1920. Lakini kabla ya hapo, hakuna chanzo chochote kilicho kuwa kimesimama kwenye hoja ya ulimwengu upo kwenye hali ya kutanuka daima zaidi ya Quran.

Wanao pinga haki, na wasiyo taka kukubali juu ya utume wa Muhammad Rehma na Amani ziwe juu yake, na wanao dai kuwa Quran siyo kazi ya MUNGU MMOJA, bali uzushi wa Muhammad, ni vipi basi wanaweza kuelezea kuwa Muhammad alikuwa ni mtu pekee kabla ya miaka ya 1920 aliyekuwa akifahamu hali ya ulimwengu ya kutanuka daima? Je kuna uwezekano kuwa kwenye miaka hiyo ya 600, Muhammad aliweza kutengeneza kifaa cha teleskop sawa na kile kilicho kuja kutengenezwa kwenye miaka ya 1920 na kuweza kuugundua ukweli huo. Je ni kweli Muhammad alikuwa na maarifa hayo ya kuweza kutengeneza Teleskop na jinsi ya kuitumia na kisha afiche iwe ni siri yake, asigundue mtu yoyote katika zama zake na hata baada ya kuondoka kwake?

Je wale ambao walimuita Muhammad kwamba ni mwendawazimu, na kwamba katika hali yake hiyo ya kuwa mwendawazimu ilimfanya ajihisi kuwa yeye ni mtume wa MUNGU MMOJA, ni vipi wanalielezea hili kwamba Muhammad alifahamu ukweli juu ya ulimwengu, ukweli ambao ulikuja kuthibitika miaka 1300 baada yakuondoka kwake?

Na wale walio dai kuwa Muhammad alianzisha dini hiyo kwa malengo ya kujinufaisha yeye mwenyewe, ni vipi wanaweza kuelezea kwamba kile Muhammad alichokisema ukweli wake na uyakinifu wake haukuweza kuthibitika mpaka baada ya miaka 1300 alipoondoka, kama ilikuwa ni kwa ajili yake mwenyewe ni vipi azungumze vitu ambavyo havitamnufaisha kwa wakati ule isipokuwa milenia moja baadaye, ambayo yeye hatokuwepo wala wale alio kuwa akiwaambia ili aweze kunufaika nao hawato kuwepo?

Wengine wanasema Muhammad alikuwa ni mtu mwenye akili mno, kiasi kwamba aliweza kuliona hili katika kipindi chake, lakini kwanza tukumbuke Muhammad alikuwa hajui kusoma wala kuandika, na pili ni mtu gani mwenye akili ambaye atavumbua kitu na kisha aseme uwongo kuwa huo siyo uvumbuzi wake, bali ni muongozo kutoka kwa MUNGU?

“Je! Hao walio kufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zime ambatana, kisha Sisi tukazibabandua? Na tukajaalia kwa maji kila kilicho hai? Basi je, hawaamini?(Quran 21: 30)

Quran inatuvuta kushuhudia ukweli mwingine wa msingi juu historia ya kuumbwa kwa ulimwengu. Kama ilivyo elezwa kwenye aya hiyo, ni kwamba mbingu na aridhi zote zilikuwa ni kitu kimoja, kabla ya kutokea kile ambacho kilipewa jina la ‘The Big Bang theory’ ambayo ilikuja kushika kasi na kufahamika miaka ya 1900. Kipindi ambacho tafiti za kisayansi zilikuwa zikipaa kwa kushindana, kipindi ambacho tafiti hizi zilikuwa ‘bize’ kutafuta nukta mbazo sayansi ili pingana na dini. 

Lakini hili la nadharia ya Big Bang ilikuwa ni pigo kwa wanametirialisti ambao waliamini kuwa ulimwengu, hauna mwanzo, na wala hauna mwisho. Big Bang ilikuwa inapaza sauti nyingine, kwamba unayo mwanzo na unao mwisho. Ukweli huu ulikuwepo kwenye kitabu cha MUNGU MMOJA, ukisubiri kwa miaka 1300 tangu ulipo tamkwa ili maendeleo ya sayansi ya binadamu yaweze kuuthibitisha. Na kama zilivyo aya nyingine za Quran, muda ulifika na dunia ilikubali kuwa maneno yaliyo semwa na mtu asiye fahamu kusoma wala kuandika, katika jangwa la Saudia, zaidi ya miaka 1400, yanayo ukweli. Swali ni moja Muhammad alijulia wapi hilo?


Katika historia hakukuwa na mwingine yeyote zaidi ya MUNGU MMOJA, kupitia kitabu chake kitakatifu cha Quran, ambacho huko ametaja tabia ya ulimwengu kutanuka daima na hatua ya kuzaliwa kwa ulimwengu wenyewe ambapo kabla mbingu na aridhi zilikuwa ni kitu kimoja. Iliwachukua wanasayansi tafiti na majaribio ya muda mrefu, wakisaidiana na vifaa bora kabisa vya kisayansi kuweza kuing’amua nukta hiyo ya msingi kwenye maisha ya ulimwengu wenyewe, na dunia iliona juhudi ya wanasayansi hao, na walitunukiwa nishani ya Nobeli kwa ugunduzi huo. Je dunia inaweza kufanya kitu kama hicho kwa Muhammad, kumtunukia nishani hiyo kwa kuweza kugundua hilo miaka 1300, kabla ya wanasayansi wa leo? Lakini kwanza ni wapi Muhammad aliupatia ukweli huu? Je alikuwa na Teleskop ambayo aliificha isijulikane kwa yeyote na aliiharibu baada ya ugunduzi wake?

Je alifanya mahesabu yahusianayo na historia ya mionzi ya anga au alituma satelaiti kabla ya hizi zilizo anza kutumwa juzi na wanasayansi wetu kwenda kuvumbua nukta hiyo? Majibu ya maswali yote haya hapana shaka ni hasi. Lakini Muhammad mwenyewe kesha sema haya si maneno yake, je ni maneno ya mashetani kama wanavyo dai wengine? Nalo jibu ni hapana, tumeona katika baadhi ya aya mashetani wenyewe wamepewa changamoto ya kushirikiana na binadamu kuandika japo sura moja, lakini hadi sasa ni zaidi ya miaka 1400 hakuna aliyeweza kufanya hivyo. Aya hiyo pia imetaja kuwa kila kilicho hai kinatokana na maji, kwa kumbukumbu tu, mwanasayansi aliyekuja kugundua hili alitunukiwa zawadi ya Nobeli, lakini miaka 1300 kabla ukweli huo ulisha tamkwa na mtu asiye fahamu kusoma wala kuandika.

"Na jua nalo linasafiri mpaka kwenye kituo chake. Hayo ni makadirio ya Mwenye nguvu, Mwenye kujua".(Quran 36: 38)

Kwa muda mrefu ilikuwa ikidhaniwa kuwa dunia haizunguki, imesimama, na kwamba kinacho zunguka ni jua ambalo linaizunguka dunia. Baadaye watu kama Copernicus, Kepler na Galileo wakaja na nadharia kuwa Jua halizunguki, na Dunia ndiyo inayo zunguka Jua. Lakini baadaye tena, baada ya tafiti na ukusanyaji wa taarifa na vielelezo mbalimbali na utumiaji wa vifaa bora kabisa vya kisayansi kama teleskop, ikafahamika kuwa Jua nalo linazunguka, dunia nayo inazunguka kulizunguka jua. Ingawa iliichukua sayansi kipindi kirefu cha makosa na usahihishaji mpaka kufikia kwenye ukweli wa msingi, Quran ilishakuwa ya kwanza kulielezea hilo miaka 1400 iliyo pita, na tangu ilipo sema hivyo hayakupatwa kubadilishwa maneno yake, wala kuonekana tofauti kwenye kile ilichokisema.

“Na unaiona milima unaidhania imetulia; nayo inakwenda kama mwendo wa mawingu. Huo ndio ufundi wa Mwenyezi Mungu aliye tengeneza sawasawa kila kitu. Hakika Yeye anazo khabari za yote myatendayo.” (Quran 27:88)
Muundo wa milima, mwonekano wake unaifanya tuidhanie kana kwamba, imetulia hapo ilipo. Aya hii inatugutusha nukta muhimu na iliyo ya msingi ya uhai wa dunia yetu. Kwamba dunia nayo inasafiri, tena kama mawingu kwa kasi mno. Kile ambacho bongo kubwa zilizo fuata baada ya Muhammad hazikuweza kukiona, ni kuwa dunia haijatulia tuli, bali nayo ipo safarini, aya zingine zimefikia kuitaja mpaka njia ya dunia na sayari na nyota zingine zinazo tumia kupita zikiwa kwenye hizo safari zao, orbiti.  Ni namna gani mchunga mbuzi katika jangwa la Arabia, asiyeweza kulisoma hata jina lake[2] aliweza kung’amua hili, ambalo baada ya milenia moja na miaka kadhaa wanasayansi wa zama zetu ndiyo wanafanikiwa kuliyakinisha?

“Anaziendesha bahari mbili zikutane (zenye maji chumvi na baridi );”
“Baina yao kipo kizuizi, haziwezi kuchanganyika.” (Quran 55: 19-20)

J. Cousteau, Mfaransa maarufu kwenye taaluma ya oceanographer, alikuwa na haya ya kusema pale alipo zungumzia suala la kizuizi baina ya bahari mbili.

“Tumeipitia kazi za watafiti fulani kuhusiana na kizuizi kinacho tenganisha bahari mbili pale zinapo kutana, na kugundua kwamba bahari ya Mediterania inayo aina yake ya chumvi na uzito tofauti, na aina tofauti kabisa ya mimea na viumbe. Kisha tukafanyia tafiti maji kwenye bahari ya Atlantiki na tukakuta vyote vinavyo patikana kwenye Mediterania pia hapa vipo, ila vikiwa na tabia tofauti kabisa na vile vya Mediterania. Bahari hizi mbili zilikuwa na tabia tofauti kabisa ingawa kwa jicho zinaonekana kugusana, lakini hazichanganyikani. ... Kipo kizuizi cha ajabu sana kinachozizuia bahari hizo mbili kukutana pamoja. Kwa kiasi kikubwa hili limetushangaza mno. ... utafiti wa kina zaidi umetoa majibu kwamba, bahari ambazo zinayo tabia tofauti (maji, chumvi,uzito, viumbe na mimea), bahari hizo zinayo kizuizi ambacho kinazizuia zisichanganyikane, ingawa zinakutana.”

Ukweli wa kimsingi juu ya tabia za bahari mbili zinazo tofautiana kwa tabia za maumbile yake, kwamba bahari hizo hazikutani, ni kitu kilicho wachanganya na kuwaacha midomo wazi wajuzi wa mambo yahusiayo bahari, yaani oceanographer wa zama zetu leo, lakini ni ukweli ambao ulishaelezwa yapata karne kumi na nne zilizo pita, na mtu kutoka jangwani, ambaye hata hana ujuzi wowote kuhusiana na mambo ya bahari. Wala hakuna rekodi kwamba alisha wahi kusafiri juu ya maji. Lakini tabia za msingi za bahari na zinazo hitaji utafiti na vifaa bora vya kileo kuweza kuzing’amua tabia hizo, Muhammad ameitaja tabia hii ya kipekee ya bahari mbili zinazo onekana kwa jicho la kawaida kuwa zinagusana, lakini kwa yakini hazifanyi hivyo, baina yao kuna kizuizi. Ni wapi Muhammad aliipata habari hii ya ndani kuhusiana na bahari?

“Ambaye amekufanyieni ardhi kuwa tandiko, na akakupitishieni humo njia, na akakuteremshieni kutoka mbinguni maji. Na kwa hayo tukatoa namna za mimea katika pea.” (Quran 20: 53)
“Na ndiye aliye itaandaza ardhi na akaweka humo milima na mito. Na katika kila matunda akafanya dume na jike. Huufunika usiku juu ya mchana. Hakika katika haya zimo Ishara kwa watu wanao fikiri.” (Quran 13: 20)
Kwenye karne ya saba, sayansi ya baiolojia ni kama haikuwepo, na mfumo wa uzalishaji kwa mimea haukuwa ni wenye kufahamika hata kidogo. Kipindi hicho ungeonekana ni mwendawazimu kusema kwenye mimea kuna yenye jinsia ya kiume na ile yenye jinsia ya kike. Lakini hicho ndicho Quran ilicho kitaja kupitia kinywa cha Muhammad. Mimea mingi inayo maumbile mfano wa yale ambayo kwa wanyama tunayaita ‘viungo vya uzazi,’ tofauti na wanyama kwa mimea ni mfano wa mbegu, ambapo kitendo cha kukutana kwao kinatambulika kama urutubishaji. Ni wazi Muhammad asingeweza kuwa na vyombo au taaluma ya mimea kiasi kuweza kutambua kuwa kwenye mimea nako kuna jinsia, swali linakuja ni wapi Muhammad alitolea haya maneno? 

Katika kipindi ambacho elimu ya baiolojia haikuwepo, vifaa vya kisasa tunavyo tumia leo havipo, ni wapi yeye alitolea taarifa hizi? Kuwa mimea nayo inayo jinsia, lakini mahala pengine Quran inasema kuwa pamejaliwa aina mbili katika kila kitu, dume na jike, chanya na hasi n.k.

“... Na unaiona ardhi imetulia kimya, lakini tunapo yateremsha maji juu yake husisimka na kututumka, na kumea kila namna ya mimea mizuri.” (Quran 22:5)

Inafahamika kuwa hakuna uhai pasina maji na hewa. Lakini je imepata kupita kwenye akili ya yeyote kuwa udongo nao unayo sehemu yake kwenye hili? Quran hapa imetaja hatua tatu muhimu kwenye maisha ya udongo. (1)Kutetema (2) kuvimba na (3) na kutoa mimea ya aina kwa aina (dume na jike)

Hatua ya kwanza mvua inapodondoka, chembe, chembe tofauti zinazo tengeneza chembe moja ya mchanga, zinaanza kutetema na kupokea au kupunguza chaji zake za kiumeme kutokana na matone ya mvua yanayo dondoka. Mwaka 1828, mtetemo huu wa udongo kutokana na matone ya mvua uliitwa ‘Brown Movement’ baada ya Robert Brown kufanya ‘uvumbuzi’ huo na kuieleza dunia kuwa matone ya mvua yanapo shuka vichembe, vichembe tudogo, tudogo, vinavyo tengeneza chembe moja ya mchanga vinatetema.

Hatua ya pili, Quran inazungumzia kuvimba au kuongezeka ukubwa kwa chembe hizo za mchanga au mchanga kwa ujumla. Chembe ya mchanga hutengenezwa na tabaka mbili, baina ya tabaka hizo kuna nafasi ambayo inaruhusu maji na chaji zinazo tokana na matone ya mvua kupenya, kisha kutokana na athari hiyo udongo unatanuka au unavimba.

Hatua ya tatu, baada ya hapo ni udongo ulio kuwa umekufa, unapata uhai, na kutoa uhai kwa mimea ambayo nayo itasababisha kupatika uhai kwa viumbe wengine akiwemo binadamu. 

Zama zote binadamu tumekuwa tukifahamu kuwa mvua ndiyo inayo sababisha mimea kuota, lakini hatukuwa hata kidogo, tukifikiria ni hatua gani au ni kitu gani kinacho tokea kabla ya mimea kuchomoza. Lakini ni vipi katika zama za Muhammadi binadamu angeweza kuzitambua hatua hizo zinazo pitiwa na udongo kabla ya kuanza kuotesha mimea yake? 

Kama tulivyo ona, hatua hii ya muhimu sana, tunaikuta inavumbuliwa mwaka 1828, na kutokana na heshima na thamani uvumbuzi huo, tendo lenyewe linapewa jina la mvumbuaji, lakini Muhammad alishakisema karne zaidi ya kumi kabla, sasa inakuwaje? Vipi Muhammad aliweza kuliona hili, ni wapi alipatia taarifa hizi, ni vipi hazipingani hata kidogo na uvumbuzi wa zama zetu?

“Na Mola wako Mlezi amemfunulia nyuki jike: Jitengenezee majumba yako katika milima,na katika miti, na katika wanayo jenga watu.” (Quran 16:68)

Quran ilipo taja suala la nyuki katika shughuli za kutengeneza asali, Quran imetaja nyuki wa kike, ndiye anayefanya zoezi zima la kuzalisha asali. Kwamba asali tunayo itumia, inazalishwa na nyuki wa kike. Lakini Quran haijaishia hapo tu ikaendelea kusema; nyuki jike ndiye anayejenga nyumba ile ambayo asali ataiweka, ndiye anaye kusanya nta, na mali ghafi nyinginezo kwa ajili ya kuzalisha hiyo asali.

Wakati Muhammad anasema kuwa yeye ni mtume wa MUNGU MMOJA, na Quran inashuka kwake, binadamu hakuwa akifahamu chochote kuhusiana na kazi zinazo fanywa na nyuki ndani ya mzinga wao. Hatukuwa tukifahamu kuwa yule nyuki ambaye anahangaika na kufanya shughuli mbalimbali ndani ya mzinga ni nyuki jike. Hatukuwa tukifahamu, wala hata kudhani kuwa kazi ya kukusanya malighafi na mpaka kuizalisha hiyo asali ni kazi ya nyuki wa kike. 

Lakini swali linakuja ni wapi Muhammad alijifunzia haya? Alijifunza kutoka kwa nani? Muhammad mwenyewe anasema, mimi siyasemi haya ila kwa idhini ya MOLA wangu, mimi si yangu haya, mimi ni mtume tu. Hivi kweli hatuwezi kuona anayo yasema Muhammad yanayo mashiko?


“Hakika Sisi tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyo changanyika, tumfanyie mtihani. Kwa hivyo tukamfanya mwenye kusikia, mwenye kuona.” (Quran 76:2)

Baada ya karne nyingi, na baada ya majaribio mbalimbali, na tafiti mbalimbali, ndipo ikathibitika kuwa, manii (shahawa) namna zilivyo, ni mchanganyiko wa vitu mbalimbali, ambavyo ndivyo vinavyo kuja kuufanya mwili wa binadamu. Quran haijatuambia ni mchanganyiko wa nini na nini unao patikana kwenye manii, karne nyingi zilizo fuata baada ya Muhammad kuondoka, majibu ya tafiti juu ya majimaji hayo, ndiyo yakaja na ni majibu ya mchanganyiko gani ambao Quran iliikusudia. 

Ilihitajika kifaa cha maikroskopi kupata majibu hayo, kupata ukweli wa maneno aliyo yasema Muhammad jangwani, maneno aliyo yasema mtu asiye faham kusoma wala kuandika. Na majibu waliyo yapata, hata nukta moja hayako tofautiana na yale aliyo yasema Muhammad. 

Kutaja kwa uchache, manii yanafahamika sasa kuwa yanamchanganyiko wa;spermatozoa, Citric acid, prostaglandin, flavins, ascorbic acid, fructose, phosphorylcoline, cholesterol, phospholipids, fibrinolysin, zinc, na acid phosphatase.

“Ati anadhani binaadamu kuwa ataachwa bure?”
“Kwani hakuwa yeye tone ya manii lilio toka kwa kuchumpa?” (Quran 75: 36-37)

MUNGU MMOJA, anathibitisha kuwa yeye ndiye aliye muumba binadamu, na anasema kuwa hatoachwa hivi, hivi, atawajibika juu ya vitendo vyake. Halafu akataja kile ambacho katika zama za Muhammad kwa namna yeyote ile kisingeweza kufahamika, mpaka kwenye zama hizi za maendeleo ya sayansi na teknolojia, anasema amemuumba binadamu kutokana na ‘tone la manii,’ maneno mawili tofauti yametumika kuelezea ukweli huo wa kisayansi. ‘maney’ (manii/shahawa) na ‘nutfah’ (tone), neno nutfah lina maana ya kile ambacho kinacho bakia katika chombo baada ya kusafishwa, hivyo ikimaanisha sehemu ya kitu na siyo kitu kizima. 

Manii au mbegu za uzazi wa kiume ambayo yanapatikana katika ule mkupuo mmoja zinapo toka huwa kiasi cha milioni 100 mpaka 200. Katika hizo mbegu zinazo fikia mamia ya mamilioni, ni mbegu moja tu pekee ndiyo, inayo kwenda kurutubisha yai. 

Hivyo kile kinacho itwa Zygote ambayo ni zao la muungano kati ya mbegu ya kiume na yai la kike ni zao la mbegu moja tu na siyo manii yote yaliyo rushwa kutoka kwenye kiungo cha uzazi cha mwanaume, na hasa ndiyo maana ya kutumika neno maalum, nutfah, katika aya hii.

Kama tulivyo ona ni mamia ya mamilioni ya mbegu za kiume ndizo zinazo tolewa na mwanaume, na kuanza safari ya kulisaka yai la kike, umbali zinayo safiri mbegu hizo katika uwiano wa microns, ni sawa na kilometa kadhaa, lakini ndani ya kiungo cha uzazi cha mwanamke safari hiyo inapo anzia, kuna vikwazo vingi, kimoja wapo ni kwamba hata hizi mbegu zinahesabiwa kuwa ni wavamiaji na mfumo wa ulinzi katika eneo hilo, hivyo zinaanza kushambuliwa hapo, kumalizwa hapo, kasi kubwa sana inahitajika kwa mbegu hizi kuweza kukwepa hayo mashambulizi, kasi hiyo zinayo safiri tunaweza kuifananisha na boti inayo safiri kwa mwendo kasi mno.

Mbegu nyingi sana na zilizo dhaifu, hufa njiani, na ‘mashujaa’ wachache ndiyo wanao weza kulifikia yai, lakini mashindano hayajaishi hapo, katika hizo ni mbegu moja tu, ndiyo itakayo ruhusiwa kulitoboa yai na kuingia ndani. Quran imetumia neno nutfah, yaani masalio yanayo bakia baada ya kile kilicho kuwemo kuondolewa, na hapa tunaona, katika mamia ya mamilioni ya mbegu hizi baada ya kufa njiani kuelekea kwenye yai, zingine zikiwa zimeshambuliwa vibaya na mfumo wa ulinzi kwenye kiungo cha uzazi wa mwanamke, na hivyo kuwa hazina faida, kile kilicho bakia, kile kilicho weza kuyashinda mazingira hayo magumu na kulifikia yai.

Tafsiri ya Nutfah tunaipata baada ya mbegu ya kiume kutoboa ganda linalo linda yai kwa kutumia aina mahususi ya enzim zilizo ndani ya kichwa cha spemu, mbegu hiyo inaanza kusafiri ndani ya ganda kulifuata yai, mashine iliyotumiwa na mbegu kulitoboa yai, enzimu, automatiki, inavunjika vunjika, kichwa cha spemu nacho kinavunjika vunjika, mkia ambao ndiyo ulitumika kama matairi kuifikisha mbegu hapo, nao unakatika, kilicho bakia kinaungana na yai, hiyo haswa ndiyo maana ya nutfah, ndiyo kilicho tumika kumuumba binadamu huyu anaye soma posti hii. 

Wewe ni mshindi ambaye katika zile mbio nyuma yako, mamia ya mamilioni eidha uliziacha zimekufa au ulizishinda kasi, na ukawa wa kwanza kudumbukia ndani ya yai, na hapana shaka bado unacho kipaji kile, kile kitakacho weza kukusaidia kuyashinda hata mazingira haya, na kuweza kuutambua ukweli ni upi na uweze kuufuata, Wewe ulikuwa mshindi, ukawashinda mamia ya mamilioni, ukiwa peke yako, leo usipumbazwe na magari, nyumba na vingine, katika mbio za mara ya kwanza vitu hivyo havikuwepo, lakini leo vipo, ila umepewa zana nyingine zaidi; akili. Basi itumie vyema akili hii kufanya uchanganuzi wa kina juu ya ukweli kuhusu MUUMBA wako.

Kutoka kwenye jangwa, mchunga mbuzi huyu, asiye jua kusoma wala kuandika, alikuwa sahihi kabisa kwenye maneno yake aliyo yasema, usahihi ambao hata baada ya karne 14 baada ya kuondoka kwake, hakuna aliyeweza kuja na kazi yenye usahihi na ukweli kama ya kwake, hakuna mahala ambapo maneno hayo yameanguka patupu. Ni wapi Muhammad aliitoa elimu hii? Alijibu Muhammad mwenyewe, haya si maneno yangu, mimi ni mjumbe na maneno haya yanatoka kwa MUNGU MMOJA, MUUMBA wa ulimwengu wote.

“Kwani hatukukuumbeni kwa maji yaliyo madhalili?”
“Kisha tukayaweka mahali pa utulivu madhubuti?” (Quran 77:20-21)

Ni sehemu gani mbegu za kiume baada ya kutolewa kwenye kiuongo cha mwanaume na baada ya kuungana na yai yanapo kwenda kukaa? Yanakwenda kukaa kwenye kizazi cha mwanamke, sehemu hiyo Quran imepataja kama, sehemu tulivu na iliyo imara. Kizazi cha mwanamke ni kama shimo ambalo limejengwa na ukuta imara. Kikawaida kizazi cha mwanamke kinakuwa na uzito wa gramu 50, katika hatua za mwisho kwenye ujauzito, lakini wakati huo kimebeba kiumbe cha uzito wa gramu 1000, wakati mwingine kichanga kinaweza kufikia uzito wa zaidi ya gramu 5000, ni kwamba mtoto anakuwa na uzito wa mara 100 zaidi ukilinganisha na kizazi chenyewe.

Ni kiungo pekee ambacho kinaweza kukuwa kwa kasi mno, kikiwa na misuli imara, migumu na iliyoshikamana barabara! Kiuongo hicho ndicho kinacho linda kiumbe ambacho nacho kinakuwa kwa kasi mno, na juu ya yote kukihifadhi kiumbe hicho na misuguano inayo tokea nje ya mwili, ndani ya chupa hilo mtoto bado anakuwa salama salimini. Quran inazipeleka fikra zetu kwenye maumbile ya kizazi cha mwanamke na tabia ya kiungo hicho na kazi inayo fanya. 

Ni nani katika zama za Muhammad ambaye angechukua maikroskopi, ambaye angeweza kufanya tafiti na kuthibitisha maneno haya? Hapana, ni mpaka katika zama ambazo sayansi inajaribu kutafuta mgongano baina ya kanuni za maumbile na yale yanayo semwa ni maneno ya MUNGU MMOJA. Lakini, kila wanapo tafuta tofauti hizo wanarudi wakiwa wameishiwa nguvu, na wale wenye kufikiri, na wale wenye akili, na wale ambao uwezo wao wa kuchanganua hauathiriwi wala kupumbazwa na vyote vinavyo tuzunguka, lazima waje kwenye nukta moja ya msingi, kitabu hichi hakukiandika Muhammad. Basi ni nani aliyekiandika? Muhammad mwenye kesha jibu, na je kuna ambaye atakayeweza kujibu swali hili zaidi ya Muhammad mwenyewe? Kasema ni maneno ya MUNGU MMOJA.

Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba,”
“Amemuumba binaadamu kutokana na Alaq (tone la damu linaloning’inia),” (Quran 96: 1-2)
“Kisha tukamfanya kuwa ni tone la manii lililoweka sehemu madhubuti.”
“Kisha tukalifanya tone hilo kuwa Alaq (tone la damu linaloning’inia) ..” (Quran 23: 13-14)

Quran hapa inaelezea hatua nyingine ya maendeleo kwenye nutfah baada ya kuungana na yai la kike. Kama tulivyo ona kupitia kwenye Quran kile kilicho patikana kwenye muungano huo kikaenda kukaa kwenye kizazi cha mwanamke. Baada ya kuungana kwa mbegu na yai zinatengeneza seli moja, ambayo nayo inagawanyika na kuwa mbili, mbili kuwa nne, mpaka zinakuwa mfano wa tone la damu lililogandamana. Ambalo linakwenda kujishikiza kwenye ukuta wa kizazi, inakaa hapo kama mfano wa kupe, yaani uhai wa seli hii mpya kuishi kwake kunakuwa sawa na kupe, imejishikiza hapo, imening’inia hapo.

Neno Alaq ni neno la Kiarabu limaanishalo kile chenye kuning’inia kwenye kitu fulani. Wakati wa Muhammad, taaluma ya embryology haikuwepo, wala hakukuwa na neno maalum kuelezea kitu fulani, lakini Quran imetumia neno ambalo, leo katika zama ambazo tunayo taaluma ya embryology, tunatumia neno maalum kuelezea hatua hiyo muhimu katika kuelekea kwenye uumbwaji wa mwanadamu, wanatumia neno Zygote, wakimaanisha kile kinacho ning’inia kwenye ukuta wa kizazi baada ya muungano wa yai na mbegu ya kiume.


Mbegu ya kiume inakutana na yai kwenye mirija ya uzazi, inayo fahamika kama fallopiantube, zikisha kutana haziishii hapo, safari inaendelea mpaka kwenye ukuta wa kizazi, inapofika kwenye ukuta huo inakwenda kujining’iniza sehemu ambayo kunayo mishipa mingi mno ya damu. Na hapo ndipo tunapo pata maana ya neno Alaq lililo tumika mahususi kwenye Quran kuelezea hatua hiyo muhimu. 

Ni vipi seli hii imeweza kutambua kuwa baada muungano wao sehemu inayo paswa kwenda kujihifadhi ni kwenye ukuta wa kizazi ambako kunayo mishipa mingi mno ya damu? Seli hiyo itakuwa na kunawiri kupitia mishipa hiyo. Itapata virutubisho vyote inavyo hitaji ili iweze kukua kupitia mishipa hiyo. Ni wapi seli hii ilipata hiyo akili au maarifa ya kufanya hivyo? Je tunaweza kukiita kitendo hicho ni natural selection? Yuko wapi Darwin atuelezee kuwa hapa kwenye hili tendo nafasi ya Natural Selection iko wapi? Je ni kitendo cha survive for the fittest? Dhana hiyo iko wapi wakati seli hiyo ilipo kuwa ikisafiri kutoka kwenye mirija ya uzazi kuelekea kwenye ukuta wa kizazi?

Kwenye safari hiyo seli hii haina kitu na muda mfupi tu ingehisabiwa kuwa ni ‘mvamizi’ na mfumo wa ulinzi ungeweza kuiulia mbali seli hiyo, kama ilivyo kwisha angamiza mamia ya mamilioni ya mbegu za kiume, na huo ungekuwa ndiyo mwisho wako, usingezaliwa, lakini ajabu seli hii inakwenda mpaka inafika kwenye sehemu yake mahususi, Quran imesema ni sehemu tulivu na madhubuti, ukuta wa kizazi, nayo inajining’iniza hapo, tena mahala penye mishipa tele ya damu ambayo itaihakikishia seli hiyo uhakika wa virutubisho vinavyo hitajika katika ukuaji wake, itakaa hapo na kuvifyonza virutubisho hivyo kama kupe, na hasa hiyo ndiyo maana ya neno Alaq lililo tumiwa na Quran. Na wakati iko hapo seli hiyo itakuwa ikitoa ina fulani ya kemikali, ili kuweza kupambana na seli hai za ulinzi za mama, ama sivyo seli hai za ulinzi zingekwisha imalizia hapo seli hiyo, na huo ungekuwa ndiyo mwisho wako.

Ni wapi seli hii imepata akili ya kujilinda namna hiyo, ili wewe uweze kuzaliwa, uone, na usikie ukweli huu, na uthibitishe kuwa wewe ni kiumbe kilicho umbwa, haukutokea kwa nasibu, na BWANA MUNGU WAKO, NI MUNGU MMOJA, ambaye kote huko tangu ukiwa tone la manii, mpaka binadamu ambaye unasoma posti hii, alikuwa, na bado yupo na ataendelea kukutizama, na mwisho wa siku utarudishwa kwake.

Mwaka 1641 William Harvey baada ya tafiti , na akiwa na maikroskopi mkononi alikuja na majibu kuwa kila kiumbe kinatokana na yai, ambalo baada ya muungano na mbegu za urutubishaji, hubadilika na kupitia hatua mbalimbali. Nao huo ulihesabiwa kama ugunduzi mkubwa. Keith Moore, profesa wa anatomy, kwenye University of Canada, kilichopo Toronto anasema kuwa, maelezo kuhusiana na embryology yanayo patikana ndani ya Quran, hayawezi kuhesabiwa kama ni matokeo ya taarifa walizo kuwa nazo watu walioishi kipindi hicho, yaani karne ya saba, hata karne kabla, hili lilikuwa halifahamiki kabisa. Ni leo tu ndiyo tupo kwenye nafasi ya kuweza kuelewa aya hizo kwenye Quran zilikuwa zikimaanisha kitu gani, tunashukuru kuwepo kwa maendeleo ya kisasa kwenye embroyology. Kwenye historia, kitabu pekee kilicho elezea maendeleo ya ukuaji wa binadamu ndani ya mfuko wa uzazi ni Quran.

Hili sisi tumeweza kulifahamu leo, kama anavyo sema profesa hapo juu, tena baada ya kuwa na maendeleo kwenye taaluma hii ya embroyology, na anakiri kuwa, hizi hazikuwa taarifa ambazo labda Muhammad alizikusanya kupitia watu wa zama zake, watu wa karne ya saba, au kabla ya hapo, hapana. Lakini ni wapi Muhammad kazitoa taarifa hizi ambazo si watu wake walikuwa nazo, wala si watu walio mtaangulia walikuwa nazo. Wala si majini, tunajua angezipatia kwa majini taarifa hizi, basi historia ingethibitisha kabisa kuwa yeye si wa mwanzo kuwa nazo, tunajua tabia yao hawa, ni kushirikiana na binadamu, na tungeweza kuzipata hizo taarifa hata kabla ya Muhammad, na hata baada ya Muhammad, tungezipata mapema, siyo kusubiri mpaka karne kumi baadaye, tena kwa msaada wa maikroskopi.

Ni wapi Muhammad alizipata habari hizi, habari kutoka kwa majini siku zote zinapingana, siku zote katika la ukweli moja wataongeza ya uwongo kumi kama siyo mia moja, lakini si kwenye kitabu hichi cha Muhammad, mpaka sasa zaidi ya miaka 1400 hakuna tulicho pata kinacho onekana ni uwongo, uzushi, au la kughushi na hakuna linalo pingana na lingine. Ni wapi Muhammad alitoa maneno haya? Kesha jibu mwenyewe, haya ni maneno ya MUNGU MMOJA.

“Kisha tukalifanya tone hilo kuwa Alaq (tone la damu linaloning’inia) na tukaiumba Alaq kuwa kama pande la nyama lililotafunwa, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa mifupa, na mifupa tukaivika nyama. Kisha tukamfanya kiumbe mwingine. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu M’bora wa waumbaji.” (Quran 23: 14)

Quran inaendelea kuelezea, baada ya kuwa Alaq kinafuatia kitu gani, inakuwa kama pande la nyama lililo tafunwa. Embroy kwenye kizazi inaonekana kama kajinyama kadogo mno kilicho tafunwa.

“Kisha kutokana na kipande cha nyama chenye umbo ambalo kiasi ni umbo na kiasi siyo umbo (la kueleweka).” (Quran 22:5)

Aya hiyo inaelezea hasa umbile linalo kuwa nayo Embroy ndani ya kizazi.
Baada ya hapo, pande la nyama lililo tafunwa ambalo umbo lake kiasi ni linaeleweka kiasi halieleweki, linageuzwa kuwa ni mifupa. Miaka michache nyuma ilikuwa ikiaminika kwamba mifupa pamoja na nyama vyote vinatokea kwa pamoja. Lakini kwa karne kumi na nne zilizo pita, ukweli huu wa msingi juu ya hatua za kimaendeleo kwa binadamu akiwa tumboni kwa mama yake zilisha elezwa kwa usahihi wake. Kwamba kwanza ni mifupa, kisha mifupa inavikwa nyama, na kisha anakuwa binadamu kamili. Ni wapi Muhammad kayatolea maneno haya?

“... Anakuumbeni katika matumbo ya mama zenu, umbo baada ya umbo, katika viza vitatu. Huyu ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Hapana Mungu isipo kuwa Yeye. Basi nyinyi mnageuzwa wapi?” (Quran 39:6)

Ujauzito ndani ya tumbo la mzazi ni kitu ambacho kinaweza kupata madhara mara moja. Kama hakukuwa na mazingira mazuri ya kiusalama, joto, baridi na mabadiliko ya hali ya hewa na hata yale anayo yafanya mama katika shughuli zake za kila  siku, yangeweza kukidhuru na hata kukiuwa kile kilichomo tumboni. Lakini zipo kuta tatu imara ambazo zinakikinga kile kilichomo tumboni mpaka muda wake utakapo fika wa kuja duniani. Kuta hizo ni (1) Ukuta wa tumbo (The abdominal wall), (2) Ukuta wa kizazi(The uterine wall), na (3) Chupa ya uzazi (The amniotic sac).

Kwa kiwango cha elimu ihusiayo mambo ya uzazi katika kipindi cha mtume Muhammad, Rehma na Amani ziwe juu yake, maelezo kama haya, hayakuwepo kipindi hicho. Hakukuwa na maarifa au teknolojia ya kuweza kuja na taarifa kama hizi. Chupa ya uzazi ambayo inakuwa imejaa aina fulani ya maji, huwa kazi yake ni kukilinda kichanga na aina yeyote ile ya mshtuko au msuguano ambao utapelekea kukigusa kichanga hicho.

Mawimbi yote ya msuguano wowote ule kutoka nje ya tumbo la mama mzazi huishia nje ya ukuta huu. Pia kuwepo kwa maji hayo kunasaidia kiumbe kilichomo humo kuweza kubadilisha mikao au nafasi kilipo, kuweza kusogeza kiguu ama kikono chake na hata wakati mwingine kanaruka ‘samasoti’ huko tumboni bila kumsumbua mama mzazi. Pasina kuwepo kwa maji hayo viungo vingine kama mikono, kichwa miguu na kadhalika visingeweza kukuwa, na hata kingebakia katika hatua ile, ile ya pande la nyama.

Quran inasema tunaumbwa kwenye umbo baada ya umbo, hili tumeshaliona, hatua ambazo tunapitia katika kuumbwa kwetu baada ya mbegu na yai kukutana na kutengeneza seli, ambayo inapita kwenye mirija uzazi na kwenda kukaa kwenye ukuta wa kizazi na kuwa seli inayo jigawanya, Zygote, au Alaq kama ilivyo kuja kwenye Quran, kisha inakuwa mfano wa damu iliyo gandamana, Alaq, kisha tunakuwa kama pande la nyama lililotafunwa, kisha mifupa, kisha mifupa inavikwa nyama, na tahamaki tumekuwa kiumbe kingine kabisa, basi Ametukuka MOLA wetu MMOJA, M’bora wa waumbaji. 

Vipi Muhammad alikuwa na chombo gani cha kuweza kumuwezesha kuziona hizi hatua za uumbaji, na akazitaja kwa usahihi wake, kama zilivyo bila kukosea hatua hata moja, kwa zaidi ya miaka 1400, yale aliyo yasema katika kipindi ambacho hakukuwa na taaluma wala vyombo vya kisasa vya kufanyia tafiti yaendelee kuwa ni sahihi mpaka leo, na yaje kuthibitishwa na taaluma zetu na vyombo vyetu vya kisasa. Ni vipi Muhammad aliweza kuona kwamba ujauzito unakaa kwenye viza vitatu, hapana rekodi yoyote kuwa alipata kufanya upasuaji na kuona hayo, leo hii katika taaluma zetu ndiyo tunathibitisha maneno ya Muhammad, ni vipi hajakosea kitu, chanzo cha taarifa hizi ni wapi? Mbona zama zake hazioneshi mwanga wowote wa kuweza kumiliki hata herufi moja ya taarifa hizi? Mwenyewe kesha sema, mimi ni mjumbe wa Allah, nami ni mtume wa mwisho katika orodha ya mitume walio tangulia, mafundisho yangu na yale ya mitume walio kuja kabla yangu hayana tofauti, BWANA MUNGU WETU, NI MUNGU MMOJA.

Tulikuwa tukiangali Quran kama kitabu cha MUNGU MMOJA, na changamoto iliyotoa ya japo kughushiwa sura moja mfano wake, na tukaona yaliyosemwa humo japo kwa uchache hayawezi kuwa ni maneno ya Muhammad mwenyewe.

Lakini kwenye Quran, kuna kitu kinacho itwa CODE, ambayo ndiyo ulinzi wa kitabu chenywe kushindwa kughishiwa au kutia mkono humo na kubadilisha maneno yake, hii nayo ni mad apana zaidi, tutaitazama kwa uchache kwenye post itakayo fuata, CODE ya Quran, na ikoje hiyo CODE kiasi hakuna Hacker aliyeweza kuihaki na kuja na mfano wa hii Quran?

Stay Tuned ...




[1]Sehemu kubwa ya nukta hii ya kuitizama Quran katika kuthibitisha uhusiano wake na MUNGU MMOJA, nimechukua kutoka kwenye kitabu cha The Quran Unchellangeable Miracle na Caner Taslaman.
[2]Katika mkataba maarufu kwenye historia ya Uislamu, mkataba wa Hudaybiyah, Waislam waliandikiana mkataba na makafiri wa Makka kipindi hicho, makafiri wale walipo soma ule mkataba waliona jina la Muhammad (s.a.w) kama mtume wa MUNGU, nao wakataka liondolewe kwenye mkataba huo, wafuasi wa Muhammad (s.a.w) wakagoma kuliondoa, basi mtume Muhammad (s.a.w) akamuomba mmoja wa wafuasi wake amuoneshe jina lake na cheo chake cha utume mahala palipo andikwa kwenye mkataba huo ili alifute kwa kidole chake mwenyewe.

3 comments: