Silka ya kumtafuta MUUMBA iliyo ndani ya roho zetu, imekuwa ikisimamia
katika vitu vitatu, mitume, vitabu na dini. Mitume au manabii wanatoa dai la
kuwa wao wametumwa na MUNGU MMOJA. Katika hao baadhi yao huja na maandiko
ambayo nayo hudai ni muongozo kutoka kwa MUNGU MMOJA, kwa ajili ya watu, na
katika maandiko hayo kinapatikana kitu kinacho itwa ni dini.
Wanao dai na walio dai kuwa ni mitume ni wengi mno, vilivyo daiwa kuwa ni
vitabu vya MUNGU MMOJA navyo vipo vingi mno, nazo dini hazihesabiki. Lakini si
kila dai limebeba ukweli. Haki ya kuumba, vilivyo umbwa na vyote vinavyo
tuzunguka, vinasimama mbele ya macho yetu na mbele ya akili yetu kama ushahidi
wa kazi ambayo kwa akili zetu hatuwezi tukaipima ubora wake, bali uwezo wetu wa
utambuzi, jicho letu, kila linapo tizama kazi za MUUMBA linarudi chini likiwa
limechoka kabisa, ni zaidi ya kile tunacho fahamu, ni zaidi ya kile kinacho
pita katika akili zetu.
Hakuna aliyekuja na kudai kokote kule kuwa kazi hii ni
ya kwakwe isipokuwa MUNGU MMOJA,kupıtıa mitume na vitabu vyake. Na hakuna
aliyejitokeza kwa ushahidi wenye kushikika au unao hata karibia kutushawishi
kwa ukweli wake au uyakinifu au njia iliyo tumiwa kukusanya ushahidi huo na
kupinga dai hilo la MUNGU MMOJA.
Dini zote duniani, vitabu vyake, mitume wake na mafunzo yake tunaweza
kuzigawa katika makundi makuu mawili, dini zile zinazo tambua juu ya kuwepo kwa
MUNGU MMOJA na zile zinazo tambua kuwepo kwa mungu zaidi ya mmoja. Nasikitika
kuwa sitaweza kuzizungumzia dini hizo kwa kila moja, hasa hizo zinazo itikadi
kuwepo kwa mungu zaidi ya mmoja kutokana na ufinyu wa nafasi ila kila mtu kwa
wakati wake anaweza kuziangalia dini hizo ambazo zinakuwa na mapungufu makubwa
matatu,
moja; asili ya mafunzo yake hayajulikani ni wapi, mbili; mgongano wa
mafundisho baina ya vipengele na vipengele, na mgongano wa mafundisho na maisha
halisi na tatu kuwa na dhana nzima ya kuathiriwa na wakati. Ingawa ukifanya utafiti bado utakutana na
mapungufu mengine mengi ambayo yatakayo kufanya uhoji uhalali na haki ya dini
hizo kuongoza maisha ya mwanadamu.
Dini zinazo kubali juu ya kuwepo kwa MUNGU MMOJA, nazo zimetofautiana
katika mambo mengi, lakini si katika msingi wa dini hizo, msingi wa dini hizo
bado uko palepale, nao ni kutambua juu ya kuwepo kwa MUNGU MMOJA, nazo ni
Uyahudi, Ukristo na Uislamu.
Pamoja na kuwepo mikanganyiko ya aina kwa aina juu ya nani hasa anayo haki
ya kudai kuwa haki ya uumbaji ni ya kwake, bado mikanganyiko na hoja hizo
hazijaweza kusimama na kuliangusha dai la MUNGU MMOJA, tunalikiri hili katika
maisha yetu ya kila siku, tunalikubali, tunalitambua, eidha kwa kutumia viungo
vyetu vya fahamu na vile vinavyo tuzunguka, au kupitia ndani ya nafsi zetu
wenyewe.
Lakini katika vitabu hivyo MUNGU MMOJA, hajatoa dai la kuwa yeye ni MUNGU
MMOJA tu, lakini pia ujumbe wake ni mmoja, nao ni HAKUNA MUNGU, ILA YEYE. Hivyo
basi mitume wote walio tumwa na MUNGU MMOJA, kote duniani, katika zama
mbalimbali nao wote walikuja na dai hilohilo, HAKUNA MUNGU, ILA YEYE.
Katika mafundisho ya msingi aliyo kuja nayo Musa (Moses), Isa (Yesu), na
Muhammad, amani ya Mungu iwe juu yao, hakuna tofauti baina ya mafunzo hayo,
wote katika mafundisho ya msingi wanasimama katika mstari mmoja, wote
wanathibitisha kuwa chanzo au asili ya mafunzo yao ni mahala pamoja.
“Amri ya kwanza ambayo MUNGU MMOJA alimpatia Musa (Moses) Amani ya Mungu
iwe juu yake, ni ‘Enyi wana wa Israeli, Bwana Mungu wetu ni MUNGU MMOJA’. Baada
miaka takribani 1350 tangu kuondoka kwa
mtume Musa (Moses), Rehma za Mungu ziwe juu yake, akaja mtume Isa (Yesu) Rehma
za Mungu ziwe juu yake, msomi mmoja katika jamii ya Kiyahudi alimfuata Isa
(Yesu) Amani ya Mungu iwe juu yake na kumuuliza, Bwana ni ipi iliyo amri ya
kwanza? Isa (Yesu) Amani ya Mungu iwe juu yake, akamjibu; ‘Enyi wana wa
Israeli, Bwana Mungu wetu ni MUNGU MMOJA’. ... Takribani miaka 600 baada ya
kuondoka mtume Isa (Yesu) Amani ya Mungu iwe juu yake, Mchungaji wa Kikristo
alikuja kwa Mtume Muhammad, Rehma na Amani iwe juu yake, na kufanya naye
majadiliano katika msikiti wa Mtume, Rehma na Amani zimshukie, wakafanya
majadiliano hayo kwa siku tatu mfululizo, usiku na mchana, katika mjadala huo,
mwakilishi wa Wakristo, alimuuliza Mtume, Rehma na Amani iwe juu yake; dhana ya
hii dini yako juu ya Mungu ni ipi? Mtume, Rehma na Amani ziwe juu yake akamjibu;
‘Sema: Mungu wako ni MUNGU MMOJA..’.”[1]
Musa/Moses na Issa/Yesu Rehma na Amani ziwe juu yao, wametajwa kwenye
kitabu kitakatifu cha Quran kama ni mitume, wote wametajwa mara nyingi zaidi
kwenye kitabu hicho kuliko hata alivyo, tajwa Muhammadi mwenyewe, Rehma na
Amani ziwe juu yake. Mitume wengine pia walio tajwa kwenye biblia wametajwa pia
kwenye Quran.
Maisha ya Isa/Yesu yameelezewa kwa kina ndani ya Quran, kuanzia kuzaliwa
kwake, kulelewa, utume na kupaishwa mbinguni.
Mama yake Isa/Yesu ambaye ni
Mariam/Mary naye si kwamba ametajwa kwa jina tu ndani ya kitabu hicho, lakini
kuna sura nzima ambayo imepewa jina la Mariam/Mary.
Lakini si hivyo tu, Quran
imemuweka Mariam/ Mary Amani ya Mungu iwe juu yake, katika daraja la juu kabisa
kupita wanawake wote duniani.
Lakini zaidi ya hapo Mariam ndiye mwanamke pekee
yake ambaye ametajwa kwa jina ndani ya kitabu hicho, Quran.
Hivyo kwa upande mmoja, tunapo tizama mitume wote ambao wametajwa ndani ya
biblia, tutawakuta pia wamo ndani ya Quran, maudhui ya hadithi zao zinaweza
kutofautiana, lakini majina na wakati mwingine matukio yanafanana, na pia
kinyume chake majina yote yaliyo tajwa ndani ya Quran, utayakuta kwenye biblia,
ila kasoro jina moja; Muhammad.
Swali linakuja ni kwa nini mitume karibu wote walio tajwa kwenye biblia
wapatikane kwenye Quran, na walio kwenye Quran wapatikane upande wa pili kasoro
Muhammad? Ni kwa bahati mbaya, kimakosa au kwa makusudi jina lake linakosekana
au Biblia haimtambui?
Wasomi wengi wa Kiislamu na hata wale ambao siyo wa Kiislam wamekuja na
hitimisho kwamba, jina la Muhammad ndani ya biblia limetajwa mara kadhaa,
lakini kutokana na ‘makosa’ ya
kufasiri kitabu hicho kuja katika lugha nyingine kumesababisha jina hilo, ‘kupotezwa’ katika tafsiri hizo.
Tofauti na Quran vitabu vilimo ndani ya biblia havipo katika lugha ya asili
ya Kiyahudi. Mathalani Biblia inayo tumika sasa kwa lugha ya Kiswahili,
imefasiriwa kutoka kwenye lugha ya kingereza ambayo iliandikwa na King James
kutoka kwenye lugha ya Kigiriki mwaka 1611.
King James naye kwake yalitoka
matoleo kadha wa kadha mpaka mwaka 1901 lilipo kuja kutolewa toleo la American
Standard Version ambalo lilitolewa kwa ajili ya nchi zinazo zungumza kingereza,
lakini ni mpaka mwaka 1952, Septemba 30, baada ya kupitia marekebisho kadha wa
kadha, na kuondolewa kwa baadhi ya vipengele na kuingizwa kwa baadhi ndipo
toleo jingine la Revised Standard Version lilipo tolewa na kupewa hati miliki,
ili asitokee mtu mwingine kuandika ‘version’ yake ya biblia.[2]
Utaona hapa tukisema tuanze kuigusa biblia na uhalali wake na haki yake
kuwa ni kitabu cha MUNGU MMOJA, itatupasa kuzama kwenye bahari nyingine pana,
ambayo itatutoa kwenye mstari wetu, nadhani kuna kazi nyingi zimeishafanywa
kulielezea hili, na wale wanao tafuta ukweli basi hawana budi kuzitafuta kazi
hizo, kwani ukweli ndiyo utakao kuweka
huru. Nilicho kuwa nataka hasa nikuangalia kwa uchache sana, yaani kidogo
sana kama kweli dai la baadhi ya wasomi kuwa jina la Muhammadi limeondolewa
kwenye biblia kwa makusudi.
Kukosekana kwa biblia ambayo ndani yake yanapatikana maneno ya asili ya
vitabu hivyo, katika lugha yake ya asili, yaani iwe ni ile ya Kiyahudi, Kiarameiki, Kiegypt
au Kimesopotamia ni mwanya mkubwa na uchochoro mbovu kabisa ambao utaruhusu
tafsiri za aina kwa aina. Kama tulivyo ona King James mwenyewe, ‘version’ yake
ya biblia na ambayo ndiyo iliyo ‘kubaliwa’ kutumika sehemu mbalimbali duniani
na kutafsiriwa katika lugha mbalimbali, ikiwemo Kiswahili, King James,
hakuitafsiri kutoka kwenye lugha ya asili, bali kutoka kwenye lugha ya
Kigiriki.
Hivyo wakati King James anaitafsiri kuja kwenye lugha ya kingereza ni
wazi makosa makubwa na yaliyo ya msingi yalifanyika.
Kitabu ambacho kitapaswa kuyaongoza maisha ya watu ili waweze kufanikiwa
hapa na maisha yanayo kuja, hapana shaka kila neno lake moja lililo tumika
limebeba dhana, uzito, maana na malengo mahususi, unapolitoa neno hilo kuja
kwenye lugha nyingine vitu hivyo na vingine lazima vizingatiwe. Haijulikani
‘version’ ya Kigiriki ilitafsiriwa na nani kuja kwenye lugha hiyo na kama kweli
wafasiri walikuwa na sifa ya kazi hiyo.
Ilipo kuja kwenye lugha ya kingereza
bado kwa karne kadhaa makosa yalikuwa yakirekebishwa, baadhi ya vitu kuondolewa
na vingine kuingizwa, ‘usahihishaji’
huu wa makosa haukuelezwa kama ulitumia vitabu vipi, vyenye lugha ipi kufanya
marekebisho hayo. Ilipo tolewa kuja kwenye lugha zingine kama Kiswahili
ilitumia chanzo cha ufasiri wake kutoka kwenye ‘version ya King James’ na siyo
nakala yenye lugha ya asili ya biblia, ni wazi makosa ya mwanzo yatakuwepo, na
mapya yataingia pia.
Kwanini biblia kitabu cha MUNGU MMOJA hakipatikani katika ‘version’ yake ya
asili. Leo hii tunao Wakristo wanao jifunza Kiarabu ili tu waweze kuifahamu
Quran vizuri kwa sababu mbalimbali, hii ni kwa vile vyovyote utakavyo ifasiri
Quran lazima tafsiri hiyo mashiko yake ya msingi ni lugha yenyewe. Yaani Lugha
ya Kiarabu na lugha ambayo unataka Quran hiyo ifasiriwe kwayo, lakini si kila
anaye fahamu Kiarabu na Kiswahili anayo nafasi ya kufasiri kitabu hicho,
hapana, walau mfasiri awe na ujuzi wa fani zisizo pungua kumi na tano ambazo
zinahusiana na mambo ya lugha. Lakini hajaishi hapo, pamoja na tafsiri
utakayoiweka, maneno yake ya asili kama alivyo yapokea mtume wa MUNGU MMOJA,
Muhammadi, Rehma na Amani ziwe juu yake lazima yawepo.
Hivyo basi si lengo langu kuzungumzia ‘uhaki’ wa biblia kuitwa kitabu cha
MUNGU MMOJA, ila nasisitiza na kupendekeza kwa yeyote ambaye anautafuta ukweli
afanye utafiti juu ya kitabu hicho, kwani kwenye agano jipya lenyewe, ambako
wanapatikana waandishi maarufu wanne, hakuna misingi ya kueleweka ni vipi waandishi
hawa waliandika vitabu hivyo na kwa nini vitabu vingine vilichomwa moto,
kufichwa, au kuondolewa katika mlolongo wa vitabu vya agano jipya na kubakizwa
hivi vinne?
Basi ni wapi ambapo Muhammadi ametajwa kwenye biblia ambako baadhi ya wasomi
kupitia makosa niliyo yataja hapo juu, wanadai kuwa limeondolewa makusudi. Hoja
hii ni nzito na vijikosa nilivyo vitaja ni vidogo mno kwa idadi lakini vizito
mno, hata hivyo bado ukitaka wingi wa idadi wa makosa hayo ndani ya biblia
fanya uchunguzi wake binafsi, kwani inakadiriwa kuwa na makosa takribani elfu
hamsini ambayo siwezi kuyataja yote hapa kwani hilo siyo mada kuu. Mada kuu
hapa ni kutafuta pale ambapo dini hizi zinapo kutana na kuthibitisha Uungu wa MUNGU MMOJA.
Ni kwa nini basi vitu hivi ambavyo vinavyo tuunganisha vimekuwa ndivyo
vinavyo puuziwa au kuto kutajwa kabisa? Kwasababu Illuminati wanafaidika na
mgawanyo huu, kama tunavyo fahamu wao, hawatambui juu ya kuwepo kwa MUNGU
MMOJA, lakini sisi tunatambua, kwa vile sisi tukiungana juu ya hili, tunakuwa
ni kitisho kwao, mafunzo ambayo daima yatatugawa kwa wao yanayo nafasi nzuri
zaidi, ili waendelee kutupotosha na kuviandika vitabu vitakatifu namna vile
wanapenda.
King James mwenyewe aliye tumiwa kuandika ‘version’ za biblia inayo
tumika hata sasa, anatokana na Bloodline ya kishetani, na hii ndiyo sababu
ukiitizama biblia kwa upande mwingine utakuta imebeba mafunzo na mafumbo pamoja
na alama nyingi za kipagani kuliko imani ya MUNGU MMOJA.[3]
“Wale tulio wapa Kitabu wanayajua haya kama wanavyo wajua watoto wao; na
kuna kikundi katika wao huificha haki na hali wanajua.” (Quran 2: 146)
“Miongoni mwa Wayahudi wamo ambao hubadilisha maneno kuyatoa mahala pake,
na husema: Tumesikia na tumeasi ...” (Quran 4: 46)
Quran hapa inatutanabahisha
kwamba, haya aliyo kuja nayo Muhammad Rehma na Amani ziwe juu yake, siyo mapya,
yanafahamika vyema kwa Wayahudi na Wakristo, tena yanafahamika vyema bila shaka
yoyote kama vile wanavyo wafahamu watoto wao, lakini kuna baadhi yao ambao
wameamua kuyaficha hayo kwa makusudi na hivyo kuwapotosha wengine.
Wamebadilisha maneno ya MUNGU MMOJA kwenye vitabu walivyo pewa na kuweka
maneno yao, na kuweka maneno ambayo wao wana yataka na kuondoa yale wasiyo
yataka na kisha kusema haya ni maneno ya MUNGU MMOJA, wakati wamesha badilisha
na nafsi zao zinashuhudia hivyo, kwamba wamesha badilisha hayo na kuingiza ya
kwao. Tutatizama kwa uchache kidogo hayo ambayo yanatajwa kufichwa na aya hii.
Lengo ni kubainisha ukweli ni upi katika haya, lengo ni kuonesha ni wapi dini
hizi tatu zinapo kutana.
Quran inakubali kuwa mitume wote waliotumwa tangu Adam mwenyewe na wote
walio kuja baada yake, wote walikuwa ni Waislamu, yaani walio jisalimisha kwa
MUNGU MMOJA. Neno ‘Islam’ pia linayo
maana ya ‘amani.’ Neno la Kiyahudi ‘Shalom’ na lile la Kiarabu ‘Salaam’ yanatoka kwenye mzizi mmoja, na
maana yake ni moja, ‘amani.’
Muhammad ndani ya Biblia Kielelezo cha 1.
“Nabii atabiriye habari za amani,
neno la nabii yule litakapo tokea, ndipo Nabii yule atakapo julikana kuwa
BWANA, amemtuma kwelikweli”. (Yeremia 28:9)
Neno ‘amani’
lililotumika kwenye aya hiyo ya Yeremia, linayo maana ileile sawasawa na neno
‘Islam.’ Utawasikia baadhi ya Wakristo wakisalimiana ‘Shalom’ yaani
wakimaanisha ‘amani,’ na Waislam wakisalimiana ‘Asalamalykum’ yaani ‘amani iwe
juu yake’, hivyo ni maneno yaleyale, yenye maana ileile, isipokuwa lugha ndiyo
tofauti.
Mitume wawili waliokuja baada ya Mussa/Moses, (a.s), yaani Issa/Yesu
na Muhammad wote wawili Rehma na Amani ziwe juu yao, wote hawakutofautiana
katika ujumbe wao. BWANA Mungu wetu, ni MUNGU MMOJA. Kuwaamini hao mitume wa
MUNGU MMOJA na mafundisho yao yote bila kutofautisha yeyote, kuamini vitabu vya
MUNGU MMOJA, kuamini Malaika wake na kuamini siku ya mwisho. Kuamini kuwa
Muhammad katika ile orodha ndefu ya mitume, ndiye mtume wa mwisho, hatokuja
tena baada yake mtume mwingine. Na hauwezi kupata kokote kwenye agano lake kuwa
Musa/Moses (a.s), kuwa ndiye mtume wa mwisho, ila tunafahamu baada yake
alifuata Issa/Yesu, (a.s).
Muhammad ndani ya Biblia Kielelezo cha 2.
“Kwa
maana BWANA wa majeshi asema hivi, Mara moja tena, ni kitambo kidogo tu, nami
nitazitikisa hizo mbingu, na hii nchi, na bahari na nchi kavu; nami nitatikisa
mataifa yote, na vitu vinavyo tamaniwa na mataifa yote vitakuja, nami nitaijaza
nyumba hii utukufu, asema BWANA, wa majeshi. Utukufu wa mwisho wa nyumba hii,
utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema BWANA wa majeshi na katika
mahala hapa nita wapa amani (shalom), asema BWANA wa majeshi.”(Hagai 2:6:9)
Hapa tunakutana na tatizo lilelile, la biblia
kuwa kwenye lugha iliyo fasiriwa tu, na maneno yake ya asili yakiwa
yameondolewa. Neno lililo fasiriwa kama ‘VINAVYO TAMANIWA’ kwenye aya ya saba ya Hagai, ambalo kwenye
biblia ya lugha ya kingereza mwanzoni limefasiriwa kama ‘TREASURE’, asili yake
kwenye biblia ya Kigiriki halikuwa ni neno, bali jina lililosomeka ‘HIMADA’
ambalo mzizi wake neno hilo ni H-M-D’, ambalo kwake tunapata jina ‘MUHAMMAD,’
lakini tangu lini majina yameanza kufasiriwa, na moja ya maana ya jina hili
‘MUHAMMAD’ ni ‘TREASURE’, sasa jina hilo lilipofasiriwa na kuja lugha ya
kingereza, kitu ambacho si sahihi, kufasiri jina, maana yake bado haikuwa
umepotea hivyo neno hilohilo lilipo fasiriwa kuja kwenye Kiswahili
wakalibadilisha zaidi, lakini ni vipi na tangu lini tumeanza kufasiri majina?
Haya ndiyo yaliyo tajwa na aya zilizo tangulia kwenye Quran, mikono ya watu
wengine iliyo tiwa ili kubadilisha maana, kupoteza maana na kuupoteza uma. Hapa
imetajwa sifa nyingine kubwa ambayo haiwezi ikawa ni kwa mtume Musa/Moses wala
mtume Issa/Yesu, (a.s), walitumwa kufikisha ujumbe wao, kwa watufulani; nyumba
ya Israeli,Musa/Moses (a.s), alitumwa kwenda kuwakomboa wana wa Israeli na
kuwapeleka kwenye nchi ya ahadi kwa ajili ya kumuabudu MUNGU MMOJA,
Issa/Yesu(a.s), aliwaonya wanafunzi wake wasiende kwenye nyumba nyingine
isiyokuwa ya Israeli. Lakini hapa huyu ametajwa kuwani ‘kwa mataifa yote.’
Hakuna mtume ambaye ujumbe wake na kazi yake inawakilisha maneno hayo kama
Muhammad, (s.a.w). Kutoka kwenye kitabu alicho kuja nacho, Quran, kutoka kwenye
hadithi zake mwenyewe, na kile tunacho kiona leo duniani kote. Uislamu ndiyo
dini pekee duniani ambayo mtu kutoka kona yeyote ya dunia anaweza kuingia
katika msikiti, na kuswali na watu wa mataifa mengine na wakaelewana, lugha ni
moja tu ya ibada kote duniani bila kujali, kabla, rangi, utaifa au bara unalo
tokea. ‘Kwa mataifa yote.’
Muhammad ndani ya Biblia Kielelezo cha 3.
“Bwana akaniambia, Wametenda vema kusema
walivyosema. Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa
ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye
atawaambia yote nitakayo mwamuru. Hata itakuwa,
mtu asiyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka
kwake.” (Kumbukumbu la
Torati 18: 18-19)
Katika
Kumbukumbu la Torati hapo juu, ujio wa mtume mwingine, mpya, unatabiriwa.
Wakristo wanaamini kuwa utabiri huo umefanywa kwa Issa/Yesu (a.s). Hata hivyo
Muhammad, (s.a.w) alikuwa katika kila hali kama mtume Musa/Moses (a.s) kuliko
ilivyo kuwa kwa Issa (Yesu).
Kunazo
tabiri kadhaa kwenye biblia ambazo zinazungumzia ujio wa mtume Muhammad
(s.a.w). Lakini nyingi ya hizi tabiri kutokana na tatizo la ufasiri au makusudi
yaliyo fanywa wakati wa kufasiri aya hizo yamebadilika.
Mfano
mzuri wa hili, ni ahadi aliyoitoa MUNGU MMOJA kwa mtume wake Ibrahim amani iwe
juu yake, kwamba ampatia taifa kubwa kupitia kwa watoto wake ambao ni Ismael na
Isaki.
Kupitia kwa Isaki, mtoto wa pili wa Ibrahim,
wametokea mitume wote wa taifa la Israeli, akiwemo Musa na Yesu (a.s), ahadi ya
MUNGU MMOJA pia ikatimilizwa kupitia mtoto mwingine wa Ibrahim, yaani Ismael,
ambaye ndiye baba wa Waarabu kutoka kwake, tunaye Muhammad, (s.a.w). Ahadi hii
ipo kwenye biblia, na imeshatimilizwa kwa pande zote mbili za watoto wa
Ibrahim, (a.s). Na siyo sahihi wanavyo fanya baadhi ya watu kwa kumtenga Ismail
na kumpendelea Isaak, wakati Biblia yenyewe inamtaja kama mtoto wa halali na
wakwanza kwa Ibrahim kupitia kwa Hajar ambaye ni mke wake wa halali.
Tunapo
itazama aya hiyo hapo juu ya Kumbukumbu la Torati.
Kitu
cha kwanza ambacho tutakitazama hapo ni neno lilitumika, ‘miongoni mwa ndugu
zao,’ kama kitabu cha biblia kinavyo tuongoza, Isaak na Ismail ni ndugu, na
kutoka kwao, mataifa mawili makubwa yakazaliwa, Wayahudi na Waarabu. Wakati
Musa ana wahubiria, aliwaambia ‘miongoni mwa ndugu zao,’ ndugu wa Wayahudi ni
akina nani? Kama mtume huyo anayebashiriwa kwenye Kumbukumbu angetokana na
Waisraeli, pasingekuwa na haja ya kusema, ‘miongoni mwa ndugu zao,’ bali
‘miongoni mwao/mwenu,’ hivyo ndugu wa Waisraeli ni akina nani au ndugu wa
kizazi cha Isaak ni akina nani? Ndugu hao ni wale wa kizazi cha Ismail, sababu
undugu upo baina ya hawa wazee wao wawili, hivyo miongoni mwa ndugu zao, ni
miongoni mwa Waarabu, ambao ndiyo ndugu zao, na kwa hao ndugu zao tunaye
Muhammad. Hawezi kuwa ni Yesu aliyekuwa anatabiriwa hapo,Yesu ingekuwa miongoni
mwao/mwenu kwa vile yeye ni Myahudi kama wao.
Muhammad ndani ya Biblia Kielelezo cha 4.
Utabiri huo umebeba mambo yafuatayo.
(i) Wana wa Israeli hawatasikia tena sauti yenye
nguvu ya Mwenyezi Mungu.
(ii) Anayebashiriwa kufika ni Nabii.
(iii)
Ataondokeshwa miongoni mwa ndugu wa Waisraeli.
(iv) Atakuwa mfano wa Musa.
(v)
Maneno atakayoyasema yatakuwa ufunuo wa Mungu.
(vi) Atawaambia yote
atakayoambiwa na Mungu. (vii) Atanena hayo kwa jina la Mungu.
(viii) Asiyetaka
kusikia maneno hayo ataadhibiwa.
(ix) Nabii wa uwongo atakayesingizia kutumwa
na Mungu atakufa.
(x) Atakayesema kwa jina la miungu wengine atauawa.
Katika Kumbukumbu
hapo juu, ujio wa mtume mwingine, mpya, unatabiriwa. Wakristo wanaamini
kuwa utabiri huo umefanywa kwa Issa/Yesu
(a.s). Hata hivyo Muhammad, Rehma na Amani ziwe juu yake alikuwa katika
kila hali kama mtume Musa/Moses (a.s)
kuliko ilivyo kuwa kwa Issa/Yesu (a.s).
Bishara
inaeleza tena ya kuwa mtume huyo atakuwa mfano wa Musa. Nasi tunaona ya kuwa
Mtume Muhammad (s.a.w.) ndiye anayeitwa mfano wa Musa katika Kurani tukufu
(sura 73:15). Yesu angewezaje kujifanya kama Musa hali mwenyewe alikuwa chini
ya Sheria ya Musa? (Mathayo 5:17, 7:12, Marko 10:19. Matendo 24:14).
Hali ya Mtume Muhammad (s.a.w.) na ya Nabii Musa
zinafanana sana. Nabii Musa alizaliwa na wazazi wawili wala hakulaumiwa katika
kuzaliwa kwake. Tena Musa alioa, alipewa Sheria mpya, alihama nchi yake baada
ya kupewa utume, alipigana na adui zake, nao wakaangamia mbele ya macho yake,
alikufa kifo cha kawaida. Hayo yote yalipatikana kwa Mtume Muhammad s.a.w. na
hivyo wamefanana kabisa. Lakini hakuna hata alama moja ya hizo inayo patikana
katika dhati ya Yesu sawa na itikadi za Wakristo.
Mtume
(s.a.w.) anaambiwa na Mwenyezi Mungu kufikisha yote aliyoteremshiwa (Quran
5.67). Yesu aliwaambia wanafunzi wake ya kuwa hatawaambia yote (Yohana
16.12-13).
Hivyo bishara hii haimhusu Yesu.
Atanena hayo kwa jina la Mungu. Mtu anayesoma
Injili anajua ya kwamba Injili yote haikuanzishwa kwa jina la Mungu. Yesu
anasema mara kwa mara.
“Bali mimi nawaambieni”(Mathayo 5:22. 28, 34.
39. 44).
Luka anasema, ameandika Injili yake kwa sababu.
“Nimeona vema mimi nami kwa kuwa nimejitafutia usahihi wa mambo hayo yote tangu
mwanzo, kukuandikia kwa taratibu, Theofile Mtukufu” (Luka 1:3-4).
Hasemi kwamba alifunuliwa na Mungu, au
ameongozwa na Roho Mtakatifu, wala hakuandika Injili hiyo ili watu wote
waisome, bali alimwandikia mtu mmoja tu, Theofile.
Paulo alisema. “Kwa habari za wanawali, sina
amri ya Bwana. Lakini natoa shauri langu” (Wakorintho 7:25).
Ni dhahiri ya kwamba lnjili za leo ni mkusanyiko
wa maneno ya watu mbalimbali. Lakini Kurani inataja jina la Mwenyezi Mungu
katika mwanzo wa kila sura, na inaonekana Mungu alikusudia kutimiza alama hiyo
waziwazi. Tena Mtume s.a.w. kabla ya kuanza kazi yoyote alikuwa anataja jina la
Mwenyezi Mungu. Na dua ya kila Mwisilamu kabla hajaanza chochote kile ni Bismillah
(Kwa jina la Mungu Mmoja)
Wapinzani
wa Uislamu wanasema ya kwamba Mtume (s.a.w.) alizua uwongo. Bishara hii
inawajibu na kusema mtu yeyote atakayemzulia Mungu atauawa. Mtume (s.a.w.)
alikaa miaka mingi duniani na akisha maliza kazi yake akafariki kifo cha
kawaida. Lakini Yesu je?
Tukifuata imani ya Wakristo kuwa aliuawa msalabani,
tunashurutishwa kusema ya kuwa (Mungu aepushe mbali) alikuwa mwongo, maana
bishara yasema kuwa nabii wa uwongo ndiye atauawa. Waislam siyo tu tunaamini
bali tunakubali kuwa Yesu hakufa msalabani, hakuuwawa, hivyo yeye si nabii wa
uongo na hivyo kufaulu kwa Mtume (s.a.w.) na maendeleo ya kazi yake ni dalili
zilizo wazi za ukweli wake.
Muhammad ndani ya Biblia Kielelezo cha 5.
“Bwana alitoka Sinai, akawaondokea kutoka Seiri,
akaangaza kutoka kilima cha Parani, na akaja na elfu kumi za watakatifu. Upande
wa mkono wake wa kuume palikuwa na sheria ya moto, moto kwao. Hakika awapenda
hayo makabila ya watu, watakatifu wake wote wamo mkononi mwako, nao waliketi
miguuni pako”. (Kumbukumbu la Taurati 33:2-3)
Hapa pameelezwa maonyesho matatu ya Mwenyezi
Mungu.Mitume watatu wakubwa wanatajwa hapa, Musa (a.s) alitoka Sinai. Seiri ni
alama ya Yesu (a.s). Na Mtume Muhammad (s.a.w.) aliangaza kutoka kilima cha
Parani. Wanazuoni wamekubali ya kwamba Parani ni kilima cha Makka .
Ajabu sana, maneno haya haya unayakuta kwenye Quran Sura 95: Aya 1-3.
Biblia
inasema. Ismail “akakaa katika jangwa la Parani” (Mwanzo 21:21)
Mtume Muhammad (s.a.w.) ni mjukuu wa lsmaili.
Mtume (s.a.w.) alipoondoka Madina kwenda kuiteka Makka alikuwa na masahaba elfu
kumi. Kabla hawajaingia Makka waliwasha moto na kila mmoja wao alibeba ili
kuwadhihirishia Makafiri wa Makka namna idadi yao ilivyo kubwa. Huo ni kweli wa
kihistoria katika maisha ya nabii Muhammad na ujumbe wake, tukio hilo lilitokea
na kurikodiwa. Lakini katika matoleo ya biblia za Kiswahili maneno yamekuwa
yakibadilishwa kila wakati.
Kwanza kwenye matoleo mengine idadi hii ya
watakatifu imetajwa kama, ‘MAKUMI YA ELFU’ badala ya ‘MAKUMI ELFU’ walipo
andika makumi ya elfu yaani waliondoa ile maana halisi inayo enda sambamba na
tukio halisi la Muhammad (s.a.w) na masahaba zake kuingia Makkah kwa idadi hiyo
na kuifanya kuwa maelfu siyo kumi bali ni zaidi ya kumi ili kuwavuruga wasomi
wa Kiswahili wanao itafuta haki wasiione, maana hapo iko wazi kabisa. Lakini hili halikutosha, katika biblia ya
Kiswahili ya Union Version ya mwaka 1952, na lile toleo la mwaka 1997
lililochapwa kwa ushirika wa Tanzania na Kenya, neno ‘MAKUMI ELFU’ limeondolewa
kabisa na badala yake wakaweka maneno ‘AKAJA MERIBATH KADESHI’ neno hili nalo
ni kuwachanganya wasomaji wa Kiswahili tu. Ingawa kwenye ile ya kingereza neno
lenye idadi hiyo limetajwa vilevile, bado hawajalibadilisha, lakini punde tu
litabadilishwa au huenda wakati unasoma post hii utakuta washabadilisha, lakini
kwenye biblia nyingi za kingereza utakuta neno hilo limeandikwa, “TEN THOUSANDS
SAINTS” yaani “watakatifu elfu kumi”, kama tulivyofasiri hapo juu.
Ni
ajabu maneno kama Tirshatha. Darkoni na
mengine yameelezwa chini katika kurasa, na mengine yameelezwa mwisho wa kitabu
cha Biblia, lakini neno Meribath-kadeshi hawakulieleza chini ya ukurasa ule
wala mwisho wa kitabu. Ingawa ni jipya kabisa lakini limefanywa lionekane kama
jina la mtu au Malaika au hivi. Wale wanaofikiri ya kwamba Biblia ya Union
Version imefasiriwa vizuri sana katika Kiswahili cha kisasa, watasemaje juu ya
uaminifu huu wa wafasiri? lilikuwaje wanazuoni wakubwa, wakubwa wa Kiyunani na
Kiebrania na Kiswahili kushindwa kufasiri au kueleza neno Meribath-kadeshi?
Inaonekana dhahiri ya kwamba dhamiri za mapadri zinawalaumu juu ya tafsiri zao
zisizo sahihi, zinazovurugwa ili kuficha haki.
Mitume watatu wametajwa hapo,
lakini sehemu ambayo wazi kabisa inaoekana kumuhusu Muhammad, pamekuwa na
tafsiri tofauti kila toleo jipya la Biblia linapo chapishwa ili kuuficha ukweli
wa kihistoria kwa Wakristo wasomao biblia ambao ukweli huo unafahamika kwa
Waislam, kwamba Muhammad, kutoka kilima cha Parani, akiwa na watakatifu makumi
elfu na kwenye mikono yao vijinga vya moto waliingia kuiteka Makkah.
Mtume alizipenda sana kabila zote. Katika
masahaba wake kulikuwa Waarabu wa makabila mbali: Wahabeshi, Waajemi na Warumi,
na Mtume (s.a.w.) aliwapenda wote. Hakuwaita mbwa na nguruwe watu wa mataifa
mengine kama alivyowaita Yesu (Mathayo 7:6; 15:26). Masahaba wa Mtume ( s.a.w.)
pia walimpenda sana. Kwa hakika Mtume (s.a.w.) alipendwa na masahaba zake zaidi
kuliko kila mtu anavyopendwa na wafuasi wake. Katika vita, kama mishale
ilipigwa kutoka katika kila upande, masahaba walimzunguka Mtume kama kuta ili
asipate kujeruhiwa. Hatuwezi kuwalinganisha na wanafunzi wa Yesu waliomtoroka
wote wakakimbia na kumwacha Yesu peke yake katika matata (Mathayo 26:56. Marko
14:50).
Muhammad ndani ya Biblia Kielelezo cha 6.
“Mpenzi wangu ni mweupe tena mwekundu -
mwekundu. Ndiye mkuu katika elfu kumi” ( Wimbo ulio Bora 5:10).
Huyu aliyetajwa hapa na Nabii Suleimani
aliyekuwa mkuu katika watu elfu kumi si mwingine bali Mtume Muhammad. Maneno ya
mbele ya haya yameeleza sifa zote za mwili wa Mtume s.a.w. kama ulivyokuwa.
Na yeyote anaweza kutafuta vitabu vilivyo elezea historia ya Muhammad na
wataona, yote yaliyo tajwa katika wimbo huu, ndizo zilizo kuwa sifa zake, hasa
rangi yake, alikuwa ‘mwekundu, mwekundu.’ Na hapo pamesemwa alikuwa ndiye
kiongozi wa ‘MAKUMI ELFU’ unayakumbuka makumi elfu? Nadhani na hili watakuja
kulibadilisha na kusema atakuwa kiongozi wa Meribath-kadeshi ... Mungu aepushie
mbali uovu huu.
Muhammad ndani ya Biblia Kielelezo cha 7.
“Atamfundisha nani maarifa? Atamfahamisha nani
habari hii? Je! ni wale walioachishwa maziwa, walioondolewa matitini? Kwa maana
ni amri juu ya amri, amri juu ya amri, kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya
kanuni, huku kidogo na huku kidogo. La, bali kwa midomo ya watu wageni, na kwa
lugha nyingine atasema na watu hawa; ambao aliwaambia, Hii ndiyo raha yenu,
mpeni raha yeye aliyechoka; huku ndiko kuburudika; lakini hawakutaka kusikia.
“Kwa sababu hiyo neno la Bwana kwao litakuwa hivi, amri juu ya amri, amri juu
ya amri; kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni; huku kidogo na huku
kidogo, ili waende na kuanguka nyuma, na kuvunjwa, na kunaswa, na
kuchukuliwa”.( Isaya 28:9-13)
Walioachishwa maziwa ni wana wa Ismail ambao
waliahirishiwa kupata ujumbe wa Mungu. Kurani tukufu iliteremshwa polepole,
amri juu ya amri, kama ielezavyo bishara hiyo. Baadhi ya sura zilishuka Makka
na nyingine Madina (Huku kidogo na huku kidogo). Kurani tukufu iliteremshwa
katika lugha ya Kiarabu ambayo ni “Midomo ya watu wageni na lugha nyingine” kwa
wana wa Israeli. Mbele imeelezwa ya kwamba Mtume s.a.w. atakimbilia Madina
kwenye raha, na mapumziko, lakini watu wa Makka watazidi kukataa ujumbe wa
Uislamu mpaka watashindwa, kuvunjwa na kunaswa, na kuchukuliwa. Na ndivyo ilivyo tokea Makkah ilitekwa na Muhammad akiwa na watakatifu Makumi elfu kama nilivyoeleza hapo juu.
Muhammad ndani ya Biblia Kielelezo cha 8.
“Naye atawatwekea bendera mataifa toka mbali,
naye atawapigia miunzi tokea mwisho wa nchi. Na tazama watakuja mbiombio upesi
sana. Miongoni mwao hakuna achokaye wala kukwaa; Hakuna asinziaye wala kulala
usingizi. Wala mshipi wa viuno vyao hautalegea. Wala ukanda wa viatu vyao hautakatika;
Mishale yao ni mikali na pinde zao zote zimepindika. Kwato za farasi zao
zitahesabika kama gumegume. na gurudumu zao kama kisulisuli. Ngurumo yao
itakuwa kama ya simba, watanguruma kama wana-simba. Naam, watanguruma na
kukamata mateka, na kuyachukua na kwenda zao salama, wala hakuna mtu
atakayeokoka. Nao watanguruma juu yao siku hiyo kama ngurumo ya bahari.” (Isaya 5:26-28).
Maelezo
ya bishara hii ni haya ya kwamba wakati utafika ambapo mtu mmoja atainua
bendera atayaita mataifa ya ulimwengu nao wataitikia wito wake na kumfuata
upesi tena kwa wingi. Wale watakao mfuata wataacha uvivu na uzembe na watajitoa
wakfu kwa imani yao. Watapigana vita na kwato za farasi zao zitatoa moto kama
risasi. Watawashambulia maadui zao kwa kasi, mfano wa kisulisuli au kimbunga.
Watawashinda maadui zao kwa njia ambayo hakuna atakayeweza kuwaokoa.
“Enyi
watu, hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu nyote ...” (Quran: 7:158).
Ni wito wake huu uliowavuta wake kwa waume kote
duniani kama nguvu za umeme. Katika uhai wake Yesu hakumbatiza hata mtu mmoja
nje ya nyumba ya Waisraeli. Vivyo hivyo. wanafunzi wake wote waliishi hatua
chache tu kutoka maskani pa Yesu. Lakini wafuasi wa Mtume wa Uislamu mwanzoni
tu, walitoka sehemu mbalimbali kama vile Yemen, Iran na Uhabeshi. Na miongoni
mwa waliosilimu alikuwemo waliokuwa zamani waabuduo masanamu, Myahudi na hata
Wakristo. Waaminio hao, (Mungu awe radhi nao), kwa kufuatia mwito wa Mtume (s.a.w.)
walijitoa kwa hali na mali kwa dini yao na wakadumu katika imani katika kila
hali hivi kwamba hata maadui wa dini ya Kiislamu wamelazimika kuusifu uthabiti
na ushupavu wa masahaba hao wa Mtume (s.a.w.) Akitukumbusha jambo hili Mwenyezi
Mungu anasema.
“Mwenyezi Mungu amewaridhia nao pia
wamemridhia,” (Quran 9:100).
Wafuasi wa Mtume walilazimika kupigana vita
kuilinda dini yao, nao humo vitani wakatumia pinde na mishale. Kwato za farasi
wao wepesi zilikuwa kama risasi na gurudumu zao kama kinyamkela. Ukali huu wa
majeshi ya Waislamu ulio tajwa hapo kwenye biblia pia umetajwa katika Kurani
tukufu kama ifuatavyo.
“Naapa kwa farasi waendao mbio wakipumua (katika
uwanja wa mapambano),”
“Na wakitoa moto kwa kupiga kwato zao chini,”
“Wakishambulia wakati wa asubuhi,”
“Huku wakitimua vumbi,”
“Na wakijitoma kati ya kundi,” (Quran 100:1-5).
Hizi
ndizo sifa za majeshi ya Waislamu na ni ajabu vile zinavyolingana na bishara
hiyo ya Isaya tuliyoitaja hapo juu. Lakini pia jingine kutoka kwenye bishara
hiyo ni suala la vita na kukamata mateka, hata sasa Uislamu imekuwa dini
isiyofahamika kwa wengi au iliyo eleweka vibaya sana na hata Illuminati kutumia
mwanya huo kujenga ‘kitisho cha Ugaidi’ kwa
jina hili la Uislamu kama tulivyo ona huko nyuma, kwa sababu tu Uislamu
kuhalalisha vita ilikujilinda na kukamata mateka.
Yesu hakufanya vita, wala
hakushika mateka, Muhammad alifanya, na hakuna aliyekuwa akisalimika, dola
zilikuwa zikitetemeka linapo ingia jeshi la Waislamu.
Muhammad ndani ya Biblia Kielelezo cha 9.
Injili ya Yohana inatuambia ya kwamba Myahudi
walitazamia ufikaji wa Manabii watatu. aliwatuma watu kumwuliza Yohana
Mbatizaji,
“Wewe
U nani? Naye alikiri wala hakukana, alikiri kwamba mimi siye Kristo.
Wakamwuliza ni nani basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule?
akajibu, La,” (Yohana 1:19-21).
Kristo, Eliya na Nabii Yule ndio Mitume watatu
waliotazamiwa kufika, waliongojewa na Waisraeli. Injili inaeleza ya kwamba
Yohana Mbatizaji ndiye Eliya, (Matt.17:10-13, Luka 1: 18), na Kristo ni Yesu.
Sasa amebaki mmoja, naye ni Nabii Yule, ambaye si mwingine ila ni Mtume
Muhammad s.a.w. maana baada ya Kristo hakuna mtu aliyedai kuwa bishara zake
zimo katika Biblia, kisha akafaulu. isipokuwa Mtume Muhammad tu.
Muhammad ndani ya Biblia Kielelezo cha 10.
Katika Yohana
14.16 imeandikwa.
“Nami
nitamwomba Baba naye atawapa Msaidizi Mwingine, ili akae nanyi hata milele”.
Tena
Yesu alisema,
“Hayo
ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu. Lakini huyo Msaidizi, huyo
Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote na
kuwakumbusha yale niliyokwambia”. (Yohana 14.25,26).
Tena Yesu alisema,
“Hata bado ningali ninayo mengi ya kuwaambia,
lakini hamwezi kuyastahamili hivi sasa. Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa
kweli, atawaongoza awaite kwenye kweli yote” (Yohana 16:12-13).
Waumini wa Kikristo wanasema “Msaidizi Mwingine”
aliyeahidiwa kufika katika Injili ya Yohana si Mtume Muhammad, bali ni Roho
Mtakatifu. Lakini kuna nukta ambazo tukizitazama haziendani hata kidogo na Roho
mtakatifu.
(i)
Kama Msaidizi huyo ni Roho Mtakatifu, Yesu
asingesema,“Yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo
Msaidizi hatakuja kwenu,”
(ii)
(Yohana
16:7).Yesu asingesema hivyo kwa sababu huyo Roho Mtakatifu wa alikuweko duniani
siku zote hata kabla ya Yesu kuzaliwa.Yesu alipobatizwa, Roho huyo alimshukia
(Math. 3:16). Tena kabla ya kuwaacha wanafunzi wake aliwapulizia, akawaambia,
“Pokeeni Roho Mtakatifu” (Yohana 20:22). Ilimradi wanafunzi wa Yesu walikuwa na
Roho huyo kabla ya kufa kwa Yesu, au tuseme, kabla hajatengana nao.
(iii) Zile alama ilizobainishwa na Yesu hazipatikani
katika Roho Mtakatifu, kama (a) kuwaongoza watu kwenye kweli yote na
kuwakumbusha maneno ya Yesu, (b) kumtukuza Yesu, alama hizo au sifa hizo ni za
binadamu ambaye;atazungumza na kuwakumbusha, atamtukuza Yesu,
hizi siyo sifa zifanyazo na roho bali binadamu. (Yohana16:14).
Mtume Muhammad s.a.w. ndiye aliyekuja miaka
mingi baada ya Yesu akileta sheria yenye amri nyingi za Sheria za zamani, na
mengi yaliyo mapya, ili kukamilisha Sheria. Kurani yenyewe inadai kuwa ni
Sheria iliyo kamili (sura 5:4.) Tena Mtume s.a.w. alimtukuza Yesu na kumkinga
na masingizio yote ya Myahudi na Wakristo, akamwonyesha kama mtu mwema asiye na
dhambi, na pia kuwa hakufa kifo cha laana msalabani.
Muhammad ndani ya Biblia Kielelezo cha 11.
“Kulikuwa na mtu mwenye nyumba naye alipanda
shamba la mizabibu, akalizungushia ua, akachimba shimo la shinikizo ndani yake,
akajenga mnara akapangisha wakulima akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa
karibu akawatuma watumishi wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale
wakulima wakawakamata watumishi wake, huyu wakampiga na huyu wakamwua, na huyu akampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumishi
wengi kuliko wa kwanza, ikawa tena vilevile. Mwisho akamtuma mwanawe kwao,
akisema watamsitahi mwanangu. Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana,
wakasemezana wao kwa wao, Huyu ni mrithi haya na tumwue, tuutwae urithi
wake,kamkamata akamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja
yule bwana wa shamba la mizabibu atawatendaje wale wakulima? Wakamwambia,
Atawaangamiza vibaya wale wabaya, na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima
wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake. Yesu kawaambia, Hamkupata kusoma
katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa
taifa lingine lenye kuzaa matunda yake. naye aangukaye juu ya jiwe hilo
atavunjika , na yeyote ambaye litamwangukia litamsaga tikitiki. Wakuu wa
makuhani na Mafarisayo waliposikia mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea
wao. Nao walipotafuta kumkamata, waliwaogopa makutano, kwa maana wao walimwona
kuwa nabii.”( Mathayo 21:33-40)
Katika methali hii iliyo nzuri Yesu ameeleza
historia ya mfululizo wa kuja kwa Mitume. Ni wazi hapa kwamba shamba la
mizabibu ndiyo ulimwengu, wakulima maana yake ni walimwengu kwa jumla, matukio
ambayo bwana wa shamba alitaka kuvuna ndiyo wema, uaminifu na ucha-Mungu,
watumishi ndiyo manabii wa Mungu waliokuja duniani mmoja baada ya mwingine;
mwana ndiye Yesu aliyekuja baada ya mfululizo wa manabii wengi. Mwana huyu
aliadhibiwa na wakulima. Baada ya kusema mambo haya, Yesu ameendelea kunena juu
ya “Jiwe” walilolikataa waashi, hilo limekuwa “jiwe kuu la pembeni.” Jiwe
lililokataliwa ndiyo wa uzao wa Ismail, waliodharauliwa na wana wa Isihaka.
Kulingana na bishara hii ya Yesu, mtu mmoja angekuwa jiwe kuu la pembeni -
“Muhuri wa Manabii,” katika lugha mashuhuri ya Qur’an tukufu - hangekuwa nabii
wa cheo cha chini, bali M’bora wa manabii atakayeleta Sheria ya mwisho na
kamili toka kwa Mwenyezi Mungu. Kuinuliwa kwa Nabii toka katika nyumba ya
Ismail lilionekana jambo geni, kwani wengi katika mfululizo wa manabii wa hapo
mbele walitoka katika nyumba ya Isihaka (Israel).
Lakini Yesu anasisitiza ya kuwa Mwenyezi Mungu
ataondoa ufalme wake kutoka nyumba ya Israeli na kuwapa wana wa Ismail,
watakaotoa matunda yake; yaani wana wa Ismail ndiyo watakaokuwa taifa
litakalodumisha ucha-Mungu na ibada ya Mwenyezi Mungu duniani. Kila mtu anaweza
kuona hapa ya kuwa hapana mtu yeyote aliyedai utume baada ya Yesu, na
akafanikiwa, isipokuwa Mtume mtukufu Muhammad (s.a.w.) Ni yeye ambaye
mafundisho yake yalihitilafiana na dini ya Myahudi na akavunja kabisa nguvu za
dini hiyo. Ni yeye ambaye taifa lake lilidharauliwa na kuchukiwa. Kama
tulivyosema hapo mbele, nabii Muhammad s.a.w. ndiye mjumbe wa Mungu wa pekee
aliyejaaliwa kushinda maadui zake wote katika uhai wake, hivyo ni yeye tu
ambaye ndiye lile jiwe ambalo yeyote aliyeanguka juu yake alivunjika-vunjika na
yeyote liliyemwangukia likamsaga tikitiki. Wakristo wamekosea sana kwa kudhani
Yesu ndiye “Jiwe” linalotajwa hapa. Lakini wanasahau ya kuwa Yesu alikuwa
Mwisraeli, hali yeye amesema Ufalme wa
Mungu utaondolewa kutoka kwa Waisraeli na kupewa taifa jingine, yaani
Waismaili.
Muhammad ndani ya Biblia Kielelezo cha 12.
“Kisha nikaona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na aliyempanda,
aitwaye muaminifu wa kweli, naye kwa haki atahukumu na kufanya vita. Na macho
yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; ...
Naye amevikwa vazi lilichovya katika damu, na jina lake anaitwa neno la Mungu...
Naupanga mkali toka kinywani mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye
atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo kwa ghadhabu
kwa hasira ya Mungu Mwenyenzi. Naye anajina limeandikwa katika vazi lake na
paji lake, MFALME WA WAFALME NA BWANA WA MABWANA.” (Ufunuo wa Yohana 19: 11-16)
Kielelezo hichi na waachia wasomaji wangu wenyewe wakifafanue, wakitafakari, wakichambue na waulize maswali ya msingi.
Ningependa kukushukuru wewe ambaye siyo Mwislamu na ambaye bado unaona kuna
haja ya kumalizia kurasa zilizo baki katika kitabu hichi. Naelewa katika
mfululizo wa kurasa za kitabu hichi, ni mengi ambayo umekutana nayo ambayo
yametikisa misingi ya imani yako, siyo kwa wasio Waislam tu, lakini hata kwa
Waislam wenyewe. Lakini fahamu kwamba kitabu hichi mwandishi kaandika kwa ajili
yako, kwa ajili ya uhuru wako, uhuru wa kiroho, kimwili na kiakili. Si kwa
ajili ya kuidhalilisha imani yako, lakini kwa ajili ya kukuonesha ni wapi wale
tunao waita viongozi wetu, wa kidini, kisiasa, kiuchumi au kijamii
wanapotuchezea na kutugawanya kwa manufaa ambayo hata wao hawatoweza
kuyadiriki. Kwa ajili ya kuonesha ni wapi zile zinazo itwa dini za MUNGU MMOJA
zinapo sema neno moja, ni yapi mafunzo ya kweli na sahihi ya mitume wote wa
MUNGU MMOJA.
Na yule ambaye atafunga safari ya kwenda kuutafuta ukweli, hapana shaka
ataupata, na je kuna lengo kubwa na lenye thamani kushinda hilo la kumtafuta
MUUMBA wako ni nani na ni kwasababu gani upo hapa? Ikiwa kweli unaamini kwamba
MUNGU MMOJA yupo, na siku ya malipo ipo, na kwamba maisha yako ya baada ya hapa
yanategemea ni kwa namna gani ulivyo ishi hapa. Hapana shaka utahitaji muongozo
ulio sahihi, muongozo kutoka kwa MUNGU MMOJA, muongozo ambao hauna chembe ya
shaka wala mkanganyiko wa japo neno moja, kwani safari unayo kwenda, haina
nafasi ya makosa. Basi utafute ukweli ulipo, usitumie akili ya kushikiwa,
muulize kiongozi wako maswali ambayo unayo uhakika anapaswa kuyajibu, na siyo
ayajibu kwa utashi wake, bali kwa muongozo sahihi, usio na shaka ndani yake,
kutoka kwa MUNGU MMOJA.
Katika mafunzo ya Kiislamu, mitume wote wanatambulika kuwa ni Waislamu.
“Mtume ameamini yaliyo teremshwa kwake kutoka kwa Mola Mlezi wake, na
Waumini vilevile. Wote wamemuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu
vyake na Mitume wake. Hatutafautishi baina ya yeyote katika Mitume wake, na
(Waumini) husema: Tumesikia na tumetii. Tunakutaka maghufira Mola Mlezi wetu!
Na marejeo ni kwako.”(Quran 2:285)
Yaani huwezi kuwa Mwislamu kama hujaamini juu ya yale ambayo alikuja
nayo Issa/Yesu Rehma na Amani ziwe juu yake, na yale walio kuja nayo mitume
wote wengine, kwani wao wote wanatoka kwa MUNGU MMOJA, ambaye ujumbe wake ni
mmoja na mafunzo yake ni mamoja, hakuna tofauti baina yao.
Wapendwa bado hatujafika mwisho kwenye safari yetu hii ya KUMTAFUTA MUNGU, Safari inaendelea, tukutane hapa next time tukiendelea na kisanga chetu ...
No comments:
Post a Comment