Leo tunaendelea na safari yetu ya kumtafuta MUNGU, lakini kwanza tumetizama
asili yetu ambayo mapak sasa bado hatujafahamu ni wapi, hivyo inakuwa vigumu
hata kufahamu ni nani aliye nyuma ya vyote tunavyoviona ikiwemo sisi wenyewe.
Sayansi imekosa lugha ya pamoja ya asili yetu ni wapi?
Leo tunaitazam roho, kitu kingine ambacho sayansi haikitambui, lakini
tunaona athari ya uwepo wake katika maisha yetu ya kila siku, huenda huku
kwenye roho tunaweza kutambua asili yetu na hatimaye kumtambua MUUMBA wetu ... tuendelee.
Tukiachana na wana NewAgers, na habari zao za zama mpya, ambazo malengo
yake ni yaleyale ya kumkana MUNGU MMOJA, hebu tujitizame wenyewe, hasa, sisi ni
akina nani?
Kila kona wapo, kwa sura tofauti, utawatambua kwa sauti yao moja, wanataka mabadiliko
mapya katika kila kitu wakati tunapo ingia kwenye zama mpya, zama za Aqurius.
Eidha tunataka kuelezea ni nini maana ya mafanikio katika nyanja yeyote au
nini maana ya kufeli katika lolote lile, au tunataka kutoa mtazamo wetu juu ya
jambo lolote lile, hapana shaka maono hayo yata athiriwa moja kwa moja na
mtazamo wetu juu ya asili ya binadamu.
Tunapo hitimisha asili ya binadamu ni
ipi, moja kwa moja tunatoa majibu yanayo husu majukumu, malengo na njia ya
binadamu ni ipi kwenye uso huu wa dunia. Lakini namna ambayo sayansi na dini
zinavyo jibu swali hili, daima mgongano unakuwepo baina ya ‘wanasayansi’ na
‘wanadini’.
Sayansi inatazama asili ya mwanadamu kama mlolongo mrefu wa ukuaji na
ubadilikaji wa maumbile, kutoka katika kiumbe duni, dhaifu, katika hali ambayo
tofauti kati ya mtu na mnyama haionekani. Hatua ambayo sayansi inamtambua binadamu
kama ni kulingana na maendeleo ya nje yanayo onekana kwa binadamu. Kama vile
kutembea kwa miguu miwili, kutumia zana na kufanya mawasiliano kupitia maneno
yanayo tengenezwa na ulimi. Hapa binadamu kwenye hii sayansi ni mtoto wa
mazingira yake mwenyewe.[1]
Lakini dini na sanaa zina elezea uumbwaji wa binadamu. Siyo mlolongo wa
evolution, bali ni kitendo cha Muumba mwenyewe. Siyo kitu kilicho pitia
mabadiliko, bali kilicho tokea kwa mara moja kikiwa kikamilifu. Dini zote na
kazi zote za sanaa zina mtambaulisha mwanadamu, siyo kama mtoto wa mazingira
yake, bali mgeni wa mazingira haya.
Ikiwa mwanadamu ni zao la mazingira yake
ama au ameumbwa, swali linalo kuja, binadamu ni nani?[2]
Wana materialisim wao wameendelea kushikilia kwamba binadamu ni mnyama
aliyekamilika. Ukuaji wa kutoka ‘mnyama’ na kwenda kuwa binadamu unatokana na
mazingira yake. Kama mwana materilist Friedrich Angels aliavyo sema,
“Mtu ni zao la mazingira yake na kazi
zake.”
Ugunduzi wa zana zake na lugha ya kuwasiliana kwa maneno ndiko kuliko
mvukisha daraja kutoka kwenye wanyama na kumfanya mtu mkamilifu.
Kwenye falsafa ya materilist mtu, ni zao la mahusiano yake ya kijamii, au
kwa uwazi kabisa ni zao la zana ya uzalishaji inayo tumika. Mtu si chochote na
hajatengeneza chochote, bali kinyume chake ni zao la mazingira anayo ishi.
Darwin akamchukua mtu huyu asiye na sifa ya ‘utu’ na akamjenga kupitia
‘natural selection’ mpaka akaweza kutengeneza zana, kuongea na kutembea kwa
miguu miwili. Baiolojia ikaikamilisha hii picha ya Darwin kwa kutuonesha kuwa
kila kitu kinarudi nyuma mpaka kwenye hatua ya kibubusa ya uhai ambapo ilikuwa
ni mgongano wa kinasibu wa kemikali zilizo sababisha uhai.
Hivyo hakukuwa na
roho, na hivyo hakuna roho na hivyo hatuna ‘mtu’ bali tuna ‘binadamu’ aliye
kuwa kupitia ‘natural selection.’
Lakini kile kilicho rekodiwa katika zama zote za historia kinacho fanywa na
binadamu, kina tofautisha sana binadamu na ‘mtu’ wa Darwin na wana matirialisti
wenzake. Picha ya wanamaterilist ni kuwa binadamu ni zao la mazingira yake,
wakati kile kinacho fanywa na binadamu kinamchora kama mgeni kwenye mazingira
yake. Mbali na kazi zinazo fanywa na binadamu kupitia ushawishi wa kidini.
Tukizitizama kazi za sanaa za mwanadamu ambazo kwa njia mbalimbali hazibebi ile
dhana ya dini bado utamuona binadamu ni mgeni katika mazingira haya, na siku
zote anajaribu kutafuta ni wapi aliko tokea.
Kulingana na sayansi mwanadamu si chochote zaidi ya mnyama aliye pewa
akili. Lakini kwa mnajibu wa dini, mwanadamu ni mnyama aliye pewa utu.
Materilist siku zote wana yaelekeza macho yetu katika vitu vinavyo onekana,
mkono siyo tu kwamba ni kiungo, bali ni zao la kazi zake. Maendeleo ya mwanadamu
kwa upande wa materilist ni yale maendeleo ya kibaiolojia na siyo kiroho.
Kwa
vile materilist wameshaikana roho tangu mwanzo, basi eidha watajitia opofu pale
wanapo ona matokeo na ‘ukuaji’ wa kiroho au hawaoni kabisa, na hivyo binadamu
wanaye mwona ni ‘mnyama’ aliye pewa akili ambayo itamuwezesha kufanya ‘natural
selection,’ na siyo binadamu aliye pewa ‘utu’ unao mtofautisha yeye na mnyama.
Lakini binadamu kumshusha na kuiweka thamani yake kwenye kazi anayoifanya,
au hitimisho lake kuwa ni ‘maendeleo’ ya kibaiolojia, hapana shaka tu tutakuwa
tumezifanyia dhulma nafsi zetu na kuzifanyia dhulma akili zetu pia.
Kama
ambavyo kazi ya sanaa haiwezi kushushwa thamani yake na kuwekwa kwenye rangi
zilizo tumika kuichora kazi hiyo, au shairi thamani yake ikashushwa ikawa ni
vina vyake.Vitu hivi viwili yaani uchoraji na shairi ni moja kati ya kazi za
sanaa, kama ilivyo sanaa na ndivyo zilivyo kazi hizi thamani yake haipo kwenye
‘vitu’ vilivyo tumika kuitengeneza kazi hiyo, bali kwenye ‘moyo.’ kwenye
‘roho,’ ya kazi yenyewe ambayo inacho kieleza hakiwezi kamwe kikaeleweka kwenye
ulimwengu wa ‘materialisim,’ roho ya kazi ya sanaa inazungumzia ulimwengu
mwingine kabisa.
Kama ilivyo nyumba ya ibada, itakuwa imejengwa na idadi kadhaa ya matofali au mawe
au chochote kile cha kuifanya nyumba hii isimame. Lakini ‘vitu’ vilivyo tumika
kujenga msikiti siyo ukweli wa mwisho kuhusiana na msikiti. Hauwezi
kuulinganisha msikiti na kambi ya jeshi, ingawa yote ni majengo. Materilist
wanamuelezea binadamu kwa kumuangalia maumbile yake ya nje. Binadamu ni kama
shairi, msikiti au kazi ya sanaa ambayo haiwezi kuelezewa na kuthaminishwa
kwenye vitu vilivyo tumika kuitengeneza. Mtu ni zaidi ya kile ambacho sayansi
zote kwa pamoja zitakavyo weza kumuelezea.[3]
Kutokana na nadharia ya Darwin ni kwamba, babu wa binadamu wa kale ndiye
alikuwa mnyama aliye endelea zaidi. Lakini hata hivyo tunapo mlinganisha babu
huyo wa kale na mnyama aliye endelea zaidi, tunakuta kuna tofauti kubwa baina
yao. Kwa upande mmoja tunaona kundi la wanyama wanao tafuta chakula na wanao
pambana na mazingira yanayo wazunguka ili waweze kuendelea kuishi;
Kwa upande
mwingine tunamuona binadamu akishughulishwa na vitu vingine zaidi ya kutafuta
chakula na kupambana na mazingira yake, tunamuona binadamu aliyezungukwa na
ibada za ajabu ajabu, anaye changanywa na imani zisizo eleweka, anaye chora
nembo za ajabu ajabu na kuzi thaminisha juu ya kila kitu. Utofauti huu hauwezi
kuelezea kwenye hatua za maendeleo ya kimwili pekee ambazo Darwin kaziita,
eveolution.[4]
Kanuni ya wanyama, au silka ya mnyama ni mfano mzuri kabisa katika usahihi
wa utendaji na tija iliyo bora kulingana na aina ya kitendo au tabia ya mnyama.
Wanyama wana utashi ulio bora sana kwenye muda, kumshinda binadamu mwenyewe.
Mathalani wanyama huacha kula saa moja kabla ya jua kuzama, nyuki huzifanya
kazi zao kwa kiwango cha juu mno cha usahihi. Maarifa na akili yana mashiko
zaidi kwenye ulimwengu wa wanyama kushinda ule wa binadamu.
“Mbali na tabia nyingi ambazo tunaweza kusema wanyama waziigiza, au
wanafanya bila hiari, lakini bado katika matendo hayo kuna mengi ambayo
hatutosita kuyapa sifa ya kiintelejinsia. Katika hili kama pale mnyama anapo
tumia zana duni kufanikisha jambo fulani au kutumia zana iliyo tengenezwa na
binadamu mwenyewe...”[5]
Sokwe anatumia fimbo kuzifikia ndizi, dubu anatumia jiwe kushambulia windo
lake. Kuna ushahidi wa kutosha wa namna sokwe, nyuki wanavyo kusanya taarifa
baina yao na kuzisambaza katika kile ambacho binadamu anakiita mawasiliano.[6]
Kwa ujumla, hakuna ambacho kinapatikana kwa binadamu ambacho hatuwezi
kukiona kwa wanyama na wadudu, kuna njia moja au zaidi ya mawasiliano, maarifa,
ustaarabu, Paka kabla ya kujisaidia huchimba kishimo kadogo, na anapo maliza
hufukia kinyesi chake, kisha hunusa kuhakikisha harufu haitoki au imekwisha,
ndipo huondoka, kunguru ndiye aliye mfundisha binadamu namna ya kuzika maiti
wake.[7] Kuna mipango ya kiuchumi kwa
viumbe wengine, mipango ya kijamii na mengine mengi.
Lakini huwezi ukakuta katika ulimwengu wa wanyama, hata kwa kulazimisha au
katika hali iliyo duni, kile kinacho itwa dini,
maajabu, sanaa, imani, ibada na mengineyo mfano wa hayo, ambayo
utayakuata kwa binadamu wa kale na wa sasa. Mnyama anapo kwenda kuwinda, hufanya
kile ambacho kwenye jicho la mwanadamu litaonekana ni kitendo cha kutumia
akili, au kitendo cha kufikiria, atanyata, atakwenda chinichini asionekane,
atashika windo lake sehemu maalum.
Lakini si binadamu, ambaye kwanza atafanya
makafara kabla ya kwenda kuwinda, mke wake nyumbani naye kuna ambayo atatakiwa
kuyafanya ili kubariki kazi yake, na asipo yafanya mumewe anaweza kuwa
matatani.
Nyuki ni mfano mzuri wa jamii na mfano mzuri wa jamii inayo fanya
kazi kwa kushirikiana, lakini nyuki hawana huruma kwa mwana jamii mwenzao
ambaye ni mdhaifu na hashiriki kazi na wenzake kutokana na udhaifu huo.
Mdhaifu
huyu hutolewa nje ya mzinga, akajifie huko. Hapa nyuki wanakosa kitu, hali au
tabia tunayoiita ni ‘utu’; tabia ambayo inaambatana na kuwalinda madhaifu na
wale wasio jiweza, tabia ya kuwapatia wengine haki ya kuishi na kuwatambua na
mengineyo.
Kwa wanyama vitu ni vile vinavyo onekana, havina maana nyingine, kwa
binadamu vitu vina maana elfu moja zaidi, na maana za ndani za vitu hivyo
ambazo wanyama wengine hawatambui. kwa binadamu maana hizo zina uzito zaidi
kushinda maumbile ya nje ya kitu chenyewe. Wakati wanyama wengine wataona pango
au mti kubwa kama sehemu ya hifadhi, binadamu ataona ni sehemu ya kutolea
makafara na nyumba ya ibada.
Ni wapi binadamu anazitoa maana hizi. Kwa nini
binadamu ambaye asili yake kama alivyoielezea Darwin kuwa ni moja sawa na
viumbe wengine achukue njia tofauti sana na viumbe wengine katika masuala yake
ya kijamii na yasiyo ya kijamii. Nadhari ya mungu binadamu kaitolea wapi,
nadharia ya kafara kaitolea wapi, nadharia ya kujitolea kwa ajili ya mwingine
na kuacha shida zake kukidhi haja za wengine anaitolea wapi, mbona hatuioni hii
kwa wanyama wenzake? ... Darwin tusaidie tafadhali.
Mambo yake na tabia zake hizi, zinamfanya binadamu aonekane ni mgeni kwenye
dunia hii kushinda wanyama wenzake. Kwanini anaamini juu ya nyota, ulimwengu
ambao hata tembo wala bluu Whales baharini hautambui. Hisia zake kubwa ni zile
za woga, lakini siyo ule waoga wa kibaiolojia ambao wanyama wengine huuhisi, ni
woga wa kiroho. Woga wa kutokuridhika, woga wa maajabu yanayo mzunguka, woga wa
ibada zake, woga wa matokeo ya vitendo vyake. Woga ulio zalisha majina ya vitu
kama ‘kitukufu,’ ‘halali,’ ‘siyo halali,’ ‘haramu,’ ‘kibaya,’ ‘kizuri,’
nakadhalika. Lakini haya yote yanatoka wapi ikiwa hapa ni kwetu na ndiko asili
yetu. Hapana binadamu ni kama mgeni kwenye uso huu wa dunia, ni kama anayo
asili nyingine, asili ya kiroho.
Kwanini mwanadamu kisaikolojia haridhiki, pamoja na kuwa atamiliki kila
kitu anacho kitaka. Kwanini pesa siyo kila kitu, atakuwa na nyumba, magari,
viwanja, biashara kubwa, kubwa, familia kubwa, na mengine na mengine, lakini
bado shimo lake la saikolojia halitotoshwa kujazwa na vitu hivyo? Kwa nini
kujiua na magonjwa ya akili vimeongezeka kila pale, hali nzuri ya maisha ilipo
ongezeka na elimu ilipo ongezeka? Kwanini maendeleo ya kivitu hayamaanishi
maendeleo ya kiutu?
Tunapo mtazama binadamu wa Darwin ni kwamba, maendeleo yake ni maendeleo ya
kibaiolojia ambayo yatatokana na juhudi zake za kupambana na mazingira yake,
mkono wake utakuwa ni bora zaidi kadiri atakavyo itumia katika kazi zake.
Misuli yake, akili na mengineyo kadiri yatakavyo tumika ndivyo ukuaji na nafasi
ya kuyashinda mazingira yake itakavyo ongezeka.
Kwa njia hiyo basi matatizo
ambayo yana mwaandama binadamu wa leo
tusinge tegemea kuyaona. Binadamu wa leo kapiga hatua kubwa sana ya kivitu na
mali kutokana na kuutumia vyema mwili wake au viungo vya mwili wake, kutokana
na Darwin huyu ndiye, ‘Perfect Man.’ Lakini mbona maendeleo hayo hayana sura ya
utu, mbona matatizo yamezidi kila hatua moja ya maendeleo ya kivitu
ilipofikiwa. Kwanini huu ulimwengu wa vitu unapingana na sehemu fulani ya
mwanadamu huyu? Ni kipi kinacho kosekana katika hii picha kubwa iliyo pambwa
kwa rangi za ‘kivitu’ za aina kwa aina?
Binadamu tunafanya mengi kufikia malengo yetu ya kivitu. Tunajinyima, tuna
wanyima wengine, tunavunja udugu, tunauwa na kumwaga damu za wengine, tunafanya
mambo kadha wa kadha ya hatari na yasiyo na utu ili kuweza kuzalisha mabilioni
na mabilioni na mabilioni ya fedha. Kukusanya utajiri kwa binadamu wa Darwin
hilo linaonekana kama lengo kuu la maisha yake, hilo ndiyo kila kitu, na
binadamu inabidi ajitoe muhanga kwelikweli kufikia hatua hiyo, atauwa,
atadhulumu, atafanya hiana, ilimradi atapitia katika kila aina ya uharibifu
kukamilisha hilo. Lakini baada ya kukusanya matrilioni ya utajiri ghafla siku
moja anakufa.
WHY DEATH, AFTER ALL THE SACRIFICE YOU HAVE MADE????
Kifo ni nini? Kwanini mtu huyu afe, kwa nini aache kila kile ambacho
alitolea jasho lake kwa bidii zake zote, aliacha usingizi wake, godoro lake
zuri, mke wake mzuri na kwenda kuuchuma huo utajiri, alidhulumu, aliuwa,
alimwaga damu na mengine kama hayo alifanya kuupata huo utajiri, lakini ndani
ya sekunde kadhaa, kama mshumaa ambao hautowashwa tena alitoweka na kuyaacha
yote hayo.Thamani ya mali hizo iko wapi mbele ya kifo. Kwanini basi asiishi
milele au walau mpaka mali aliyo yachuma yamalizike.
Kama kukusanya utajiri na
mali ndiyo lengo kuu kama Darwin anavyo tuelekeza, na binadamu huyu kayapitia
makubwa kuukusanya huo utajiri, mwishowe kafanikisha, iweje basi anakufa
anauacha? Tayari kesha timiza lengo, inamaana malipo ya kutimiza lengo lake ni
mauti? Au kuna ambacho Darwin hatuambii, au kuna ambacho Darwin katika nadharia
yake amekiruka bila kutueleza. Huyu binadamu alistahiki abaki atumie mali yake
ambayo ndiyo lilikuwa lengo kuu la maisha yake, lakini sasa anaiacha na
anakwenda ambako hata hatupajui.
Lakini hata yule ambaye ameshindwa kulifikia
lengo hilo la Darwin, yaani masikini naye anakufa, sasa tofauti yao ni ipi kati
ya yule alitekeleza lengo na kuwa tajiri na yule aliyeshindwa na kuwa ni
masikini?
Hivi Darwin anatuambia ni kitu gani kinacho fuata baada ya binadamu kufa.
Lakini kwanza kwa kuanzia kifo ni nini? Darwin hawezi kutuambia kifo ni nini
kwa vile binadamu wa Darwini anacho kiwiliwili tu na hana roho. Ndiyo maana maendeleo
ya binadamu huyu yanapimwa kivitu kama hatua ya maendeleo ya kiwiliwili hicho
na siyo kiroho.
Kama hana roho unadhani Darwin ataanzia wapi kuelezea maana ya
kifo. Binadamu anakwenda wapi baada ya mauti. Ingawa Darwin anajaribu
kutushawishi kuwa hatuna roho na bila kutoa ushahidi wowote, hatuwezi
kuyachukua maneno yake kama ukweli wa msingi dhidi ya kile ambacho kiko wazi
kama nuru ya jua katika uhakika wa kuwepo kwa roho.
Darwin anataka tukatae uwepo wa MUNGU, lakini kwanza anatufundisha kukata
juu ya kuwepo kwa roho na juu ya kuwepo kwa kifo kwa sababu ni roho ndiyo inayo
mtaambua MUNGU na siyo mwili wa Darwin, hivyo tukiweza kuikana roho kuwa haipo
moja kwa moja kifo kitakuwa hakipo, na moja kwa moja maana ya uwajibikaji wa
matendo yetu itafutika, na MUNGU naye atafutika pamoja na hayo katika maisha
yetu.
Lakini ni vipi tunaweza kuikana roho/nafsi yetu. Mpaka leo sayansi haina
tafsiri inayo eleweka juu ya kifo, na vipi wataipata tafsiri yake ikiwa kwenye
kamusi zao hakuna ‘roho’ wala ‘kifo’ chenyewe.
Binadamu anayo roho, hayawani wengine na viumbe wengine wanayo roho pia,
kwani hii ndiyo hasa sababu tunatumia neno ‘viumbe/kiumbe’ yaani kilicho umbwa
na chenye uhai.
Lakini binadamu anayo, ‘uhuru’ ambao akiutumia vyema roho yake
hiyo itakuwa na hadhi bora kushinda ile ya Malaika, na anapo utumia ambavyo
sivyo atakuwa ni duni kuwashinda hayawani wengine. Roho/Nafsi ndiyo yenye silka
ya kumtambua MUUMBA. Mbali na mwili roho/nafsi ndiyo yenye mamlaka juu ya mwili
na yenye kuwajibika juu ya uhuru alio milikishwa mwanadamu na majini juu ya
viumbe vyote.
Katika mafunzo ya Kiislamu tunajifunza kuwa siku ambayo MUUMBA
atawasimamisha viumbe vyake na kutoa hukumu, siku hiyo viungo vya mwanadamu
vitatoa ushahidi juu ya roho/nafsi yake kuwa ilifanya kadha wa kadha. Hii
inatuthibitishia kuwa, roho/nafsi na mwili ni vitu viwili tofauti, na siyo
mwili ambao Darwin kautilia msisitizo wenye jukumu la kumtambua MUUMBA, bali ni
roho/nafsi ndiyo yenye jukumu hilo na mwili wake ni zana itakayo muwezesha
kuutambua ukweli huo, ingawa roho/nafsi inayo wazo, dhana, silka juu ya kuwepo
kwa MUUMBA, itautumia mwili wake na vile vinavyo mzunguka kuthibitisha hilo, au
kutumia kiburi chake kulikataa hilo.
Kwani nafsi/roho yenyewe kuwepo ndani ya
mwili, na kufikishwa hapa duniani, sehemu ngeni kwake, lakini inayo ‘fahamika’
zaidi na mwili wake ni dalili tosha kuwa yenyewe siyo ya hapa, na daima
binadamu wa zama zote amekuwa akijiuliza swali moja, asili yake ni wapi, swali
hili haliulizwi na ubongo, bali nafsi/roho, kinacho fanya ubongo kama sehemu ya
mwili ni kuisaidia nafsi kuutambua au kuuthibitisha ukweli huo.
Mathalani imetokea mahala nyumba inaungua moto, pakasikika sauti ya
kichanga ndani ya nyumba inayo waka moto, akatokea mtu mmoja akavua shati lake
na kujitosa ndani ya nyumba inayo waka moto kwa nia ya kukaokoa kachanga hako.
Baada ya muda ‘shujaa’ huyo anatoka akiwa na kachanga hako mkononi, lakini
tayari kameshakufa. Hakufanikisha lengo la kuokoa maisha ya kachanga hako, je
ni nini thamani ya kitendo hicho cha kishujaa ikiwa mtoto alikufa?
Kwanini
tunakiita ni kitendo cha kishujaa, wakati kichanga kimetolewa kikiwa kimekufa?
Kiungo cha mwili kinacho itwa ubongo kitachora picha ya kushindwa kwa mpango mzima,
kuto kufanikiwa kwa mwokoaji ndiko kunako onekana kwenye kiungo kinacho itwa
ubongo, lakini yule mwenye dhamana ya ubongo huo, yaani roho/nafsi kwake thamani
haiko kwenye matokeo, kwake mwokoaji ni shujaa.
Jina au sifa ya ushujaa
haitafsiriwi na ubongo bali nafsi yenyewe, hii ndiyo maana pamoja na kwamba
tendo halikufanikiwa, bado mtu huyu aliye jitolea maisha yake kuokoa maisha ya kichanga
ataonekana ni shujaa.
Ubongo hauwezi kutafsiri maana ya ‘shujaa’ ila nafsi/roho ambako kitendo
cha kuokoa maisha ya kitoto ndiko kilicho pewa jina la shujaa. Hata tunapo
kataa juu ya kuwepo kwa roho/nafsi bado bila kujijua au kwa kushindwa na namna
ni mengi ambayo tunashindwa kuyaelewa kwa kutumia ‘akili’ na kuyarudisha kwenye
asili yake, nayo ni roho/nafsi. Kwa mnasaba wa roho/nafsi kitendo cha kuokoa
maisha ya kichanga kilisha fanyika, hata kabla ya mwokoaji kuingia ndani ya
nyumba inayo waka moto.
Kanuni hii muhimu inayo fahamika kwenye roho/nafsi zaidi kuliko kwenye
ubongo imeelezewa vyama pia kwenye mafunzo ya Kiislamu, pale mtume Muhammad
(s.a.w) aliposema kuwaambia wafuasi wake;
“Kila kitendo kinalipwa kutokana na nia ...” [8]
Kutokana na mafunzo ya hadithi hii ni kwamba, endapo mtu alinuia kwenda kumsaidia mtu mwingine kwa lolote lile jema, lakini akafika na kukuta muhusika shida yake ilishakwisha, hivyo hahitaji tema msaada wowote, MOLA wake mtu huyu anaandikiwa kuwa alishamsaidia muhusika na atandikiwa thawabu moja kama mtu aliyetekeleza wema huo kwa ukamilifu.
Katika mafunzo ya Kiislamu pale ambapo maji yame kosekana kwa ajili ya Mwisilamu
achukue udhu, au anayo matatizo ambayo kwa yeye kushika maji kutamletea madhara
zaidi, hana budi Mwisilamu huyo kufanya Tayamamu. Yaani Mwislamu atachukua
mchanga, kisha atapiga viganja vya mikono yake juu ya mchanga huo na kisha
kuikung’uta mikono yake, vumbi lililo bakia kwenye viganja vya mikono yake
atalitumia kujipangusia uso wake na mikono yake miwili na hapo atakuwa amejitaaharisha
(amejisafisha) tayari kwenda kuswali, tayari kusimama mbele ya MOLA wake.
Lakini ni namna gani mchanga unaweza kumsafisha mtu, hata Waislamu wengi bado
wanakuwa na wasiwasi juu ya tendo hili, lakini lazima wawe na wasiwasi, kwa
vile amri ya kutumia mchanga kama njia ya kujisafishia na kama zilivyo amri
zingine zote hazikutumwa au haziku amrishwa, akili/ubongo wa binadamu, bali
nafsi/roho. Ni mengi kwenye masuala ya dini ambayo akili haiwezi kuyaelewa, kwa
vile akili ni zana tu, na nafsi hasa ndiyo inayo lengwa.
Kwenye sheria zetu za kimahakama, mtuhumiwa wa mauwaji anasimama baina ya
‘vizimba’ viwili, eidha kauwa kwa bahati mbaya au kauwa kwa kukusudia. Adhabu
ya kuua kwa kukusudia inakuwa ni kali na mara nyingi ni kifo, wakati ile ya
kuuwa kwa bahati mbaya inakuwa ni kifungo maalum au faini na wakati mwingine
vyote. Lakini tunajuaje kuwa alikusudia au ni bahati mbaya?
Mara nyingi hakimu
hutafuta namna yoyote ile au mazingira yoyote yale yatakayo wezesha
kumfahamisha NIA ya muuaji ilikuwa ni ipi. Hapa hakimu hatizami mwili wa
mtuhumiwa, bali roho yake. Je roho yake ilikuwa na dhamira ya kufanya kitendo
hicho ama la. Kwa sababu kama roho/nafsi ya mtuhumiwa iliisha dhamiria kufanya
kitendo hicho, kwa maneno mengine, kama ambavyo roho ya shujaa iliisha kiokoa
kichanga kile kabla shujaa hajaingia ndani ya nyumba inayo waka moto, ingawa
kichanga kilitoka kikiwa kimeshakufa kwenye mikono yake, ndivyo hivyo, hivyo
kuwa roho ya mtuhumiwa iliisha muuwa mhanga wake hata kabla muuaji
hajakamilisha tendo hilo.
Sheria zetu wenyewe zina tuthibitishia kuwa kuna
zaidi ya mwili wa binadamu, kuna roho, ambayo inawajibika, kuna roho iliyo pewa
dhamana, kuna roho iliyo umbwa, nayo hiyo roho haina budi kumtafuta MUUMBA wake
wa haki, na siyo mwili wake wenye jukumu hilo.
Ingekuwa hakuna roho, ni vipi hakimu angeweza kujua kwamba muuaji
alikusudia au alifanya bahati mbaya? Ingekuwa hakuna roho ni vipi kitendo cha
kutoka na kichanga kilicho kufa kwenye mikono ya mtu aliye weka rehani afya na
hata uhai wake kuokoa maisha ya kichanga hicho, kitendo hicho kiitwe ni cha
kishujaa? Wapigania uhuru wa nchi zetu, tunawahesabu ni mashujaa, ingawa
wamelala chini wamekufa, ushujaa wao uko wapi? Ubongo unaweza kutupa tafsiri ya
neno shujaa? Hapana, neno shujaa ni hali inayo jaribu kuelezwa na ubongo wetu
kwa msaada wa mazingira yetu, lakini maana yake inafahamika zaidi kwenye
nafsi/roho zetu kuliko bongo zetu.
Tofauti na dunia inayo tuzunguka, ambapo wamo matajiri na masikini, wajinga
na wenye akili, wenye busara na wapumbavu, wenye elimu na wajinga, wenye nguvu
na madhaifu. Hali zote hizi hazielezi maana ya kweli ya nafsi/roho zetu. Dunia
yetu ya ndani au kwa maneno mengine nafsi/roho zetu zimejengwa kwa uhuru na
usawa ambao hauna mipaka ya kivitu au kiasili.
Ulimwengu wetu wa ndani unajieleza wenyewe kupitia nia zetu na hamu. Kila
binadamu anayo maono ya kuishi kwa furaha ndani ya nafsi yake. Mfano watu wengi
hawawezi kuondoa uovu, lakini wana chukia uovu na wanaupinga ndani ya
nafsi/roho zao na katika msingi huo ndipo inapo patikana maana ya toba. Utu
haupo katika vitendo; bali kwenye hamu na nia ya kuishi kwa wema. Siyo
ubinadamu kutokuwa mkosaji wala mtenda maovu. Bali kukosea na kutenda maovu,
kisha ukatubia ndiyo kuwa binadamu. Mtume Muhamadi (s.a.w) amesema kila
binadamu ni mkosaji na aliye M’bora wa wakosaji ni mwenye kutubia. Mwenyewe
Mtume (s.a.w) alikuwa akitubia kwa siku mara mia moja ama zaidi, mbali na kuwa
MOLA wake alisha muambia kuwa amemsamehe makosa yake yaliyo pita na yatakayo
kuja katika maisha yake. Yeye alikuwa ni binadamu na mara kadhaa mwenyewe
alilisisitiza hilo kwa wafuasi wake.
Ni vitu vingapi ambavyo tumevifanya na ambavyo hatukuwa tukitaka au penda
kuvifanya? Na vipo vingapi ambavyo tuna nia na kutamani kuvifanya lakini bado
hatujaweza kuvifanya? Zipo dunia mbili, ile ya kivitu na ile ya kiroho. Nia
zetu, hamu zetu, ingawa hatuja zitimiliza katika dunia yetu ya kivitu, zilisha
timilika katika dunia yetu ya kiroho, hivyo, hivyo kitendo cha bahati mbaya,
kama muuaji aliyeua bila kukusudia, ingawa kitendo kile kimefanyika katika ulimwengu
wa kivitu, hakikubaliki na hakija fanyika katika ulimwengu wa kiroho, na sheria
zetu za kimahakama zinalitambua hili.
Mahusiano baina ya “hamu” na “kitendo” yana kinzana kama ambavyo mahusiano
baina ya mwili na roho yanavyo kinzana. Katika maisha yako ya kila siku utakuwa
unasikia watu wakisema na hata wakati mwingine wewe mwenyewe ukisema, “ningependa
kufanya, lakini roho yangu inasita ...”
Nia na kitendo, roho na mwili ni dunia mbili tofauti. Moja thamani yake
inaonekana kwa macho, nyingine thamani yake imehifadhiwa katika roho/nafsi za
watu na ikihusishwa na ulimwengu mwingine kabisa; moto na pepo. Huko ndiko muuaji
wa kukusudia ambaye sheria katika ulimwengu wa vitu, imekuwa ni ‘fupi’ mno
kiasi haikuweza kumfikia, na shujaa ambaye ametaka kuokoa kichanga kwenye
nyumba inayo waka moto hakufanikiwa kukiokoa na kwenye macho ya ubongo
akaonekana kushindwa, katika dunia nyingine ya Moto na Pepo vitendo vya hao
wawili vinayo malipo yake.
Katika kila binadamu kuna sehemu ndani, inayo fahamika kama nafsi au roho.
Neno hili lugha ya Kiswahili imelichukua kutoka kwenye lugha ya Kiarabu, na
tafsiri yake inayo maana pana zaidi na kueleweka zaidi katika lugha hiyo kuliko
Kiswahili, lakini juu ya yote neno hilo ndiyo ile nukta ya kati, au neno la
mwisho au mstari wa mwisho katika kila kiumbe. Katika lugha yetu hakuna tofauti
kati ya nafsi na roho. Nia inayo maana kwenye roho/nafsi, nia inamanisha
maamuzi yaliyo kwisha fanywa ndani ya mtu binafsi, siyo kwenye ubongo wala
kwenye kiungo chochote kile, bali ndani ya roho yake, ndani ya nafsi yake.
Roho/nafsi siyo kiungo bali ... kiumbe.
Hivyo kitendo ni uthibitisho au
uhakikisho au utimilisho wa kile ambacho kilisha amuliwa na kupitishwa ndani ya
nafsi/roho. Kitendo hicho kinaweza kwenye dunia ya kivitu, kufanyika au
kutokufanyika, lakini katika ulimwengu wa roho, ndani kabisa kwenye nafsi yako
kilisha kwisha kufanyika, tena mara moja na tena kitadumu hivyo milele.
Kitendo
chochote cha binadamu ambacho hakijafanyika ndani yake kwanza, ni sawa na
kitendo cha mashine yeyote ile unayo ifahamu. Mwenye ugonjwa wa akili akiuwa
hapatwi na hatia ya kitendo hicho, bali atakwenda kutibiwa kwanza tatizo la
akili, kwani kitendo alicho kifanya hakina tofauti na mashine, hakijafanyika
ndani yake, bali katika ubongo wake.
Mtu siyo kile anacho kifanya, bali kile anacho tamani kukifanya.[9]
“Naapa kwa jua na mwangaza wake! Na kwa mwezi unapo lifuatia (jua)! Na kwa
mchana unapo lidhihirisha! Na kwa usiku unapo lifunika! Na kwa mbingu na kwa
Aliye ijenga! Na kwa ardhi na kwa Aliye itaandaza! Na kwa nafsi na kwa Aliye
itengeneza! Kisha akaifahamisha uovu wake na wema wake. Hakika amefanikiwa
aliye itakasa (hiyo nafsi).Na hakika amekhasirika aliye iviza (hiyo nafsi).(Quran
91:1-10)
Darwin alipo taka kumkataa MUUMBA, kwanza aliikataa nafsi/roho, na sisi
tumejaribu kuitafuta nafsi/roho, ingawa kwa uchache, lakini tumeona uthibitisho
juu ya kuwapo kwa nafsi/roho. Kukubali kuwepo kwa roho ni kukubali kuwepo au
kupatikana kwa kitendo cha uumbaji nako ni kukubali kuwepo kwa MUUMBA. Tabia na sifa za roho zinatuelekeza
kule alipo MUUMBA.
Ikiwa roho zetu zinakiri juu ya kuwepo kwa MUNGU MMOJA WA HAKI. Je ni upi
ushahidi ambao roho zetu zinajaribu kutuelekezea ambapo viungo vyetu hasa akili
zetu zitusaidie katika kuthibitisha madai yanayo tolewa na roho zetu? Je MUUMBA
amejitokeza kukiri dai linalo letwa na roho zetu kuwa yeye ndiye MUUMBA wa
ulimwengu huu na vyote vinavyo tuzunguka zikiwemo roho na miili yetu?
HEY ... MTANANGE UNAENDELEA HAPA HAPA ... MPAKA TUFIKE TUNAPOKWENDA ...
Somo lako n pana na kubwa mnoo mungu akulipe kheri
ReplyDelete